2691; Umefika mpaka hapo, unaweza kufika mbali zaidi.

Unapokuwa utajifunza mambo mapya, ni rahisi kuona kama umechelewa sana.
Unaweza kujiambia kama ungeyajua hayo mapema basi ungekuwa mbali zaidi.

Hali hiyo inaweza kufanya uone huna cha kufanya kwa sasa, kwa sababu umeshapoteza sana.
Ni hali inayoweza kukukatisha tamaa.

Lakini hivyo sivyo inavyopaswa kuwa, hali ya kujifunza mambo mapya ambayo hukuwa unayajua inapaswa kukupa moyo.

Kwamba kama huko nyuma hukuwa unayajua hayo mazuri, na bado uliweza kwenda mpaka kufika pale ulipo sasa, kwa kujua hayo mazuri utaweza kwenda mbali zaidi.

Hebu pata picha umekuwa unaendesha biashara kwa miaka mingi bila kujua kuhusu namba za biashara, masoko na kudhibiti mzunguko wa fedha.
Lakini biashara hiyo haijafa.
Hiyo ina maana ukianza kuyatumia hayo unayojifunza, biashara yako itakua kuliko ambavyo ipo kwa sasa.

Kama ulikuwa huyajui mengi na bado umefika hapo ulipo sasa, pata matumaini makubwa kwamba kwa mengi unayojifunza, ukiyatumia utapata makubwa kuliko ulivyokuwa unapata huko nyuma.

Hatua ya kuchukua;
Ni mambo gani mapya unajifunza na kujiambia umechelewa?
Kuanzia sasa usijiambie tena hivyo, badala yake ona jinsi mambo mapya unayojifunza yanavyokwenda kukufanya uwe bora zaidi ya ulivyokuwa huko nyuma kitu kitakacholeta matokeo makubwa zaidi.

Tafakari;
Kama kuna mengi ulikuwa hujui wala kufany lakini umefika hapo ulipo sasa, hebu pata picha ukijua mengi mapya na kuyafanyia kazi utafika wapi.
Kila unapojifunza kitu kipya, pata shauku ya kukifanyia kazi kwa sababu unajua kitakufikisha mbali zaidi.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining