2692; Muda, nguvu na umakini ni ule ule.
Ukiwa na malengo madogo, muda wako wa siku utakaofanya kazi ni ule ule, nguvu zako za mwili utakazotumia ni zile zile na umakini utakuwa ule ule.
Ukiwa na malengo makubwa, bado muda, nguvu na umakini utakaotumia ni ule ule.
Malengo madogo ni rahisi kuyafikia, lakini hayabadili chochote kwenye maisha yako.
Malengo makubwa ni magumu kuyafikia, lakini yanaleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.
Na hata kama hutayafikia malengo hayo makubwa, bado matokeo utakayoyapata yatakuwa tofauti na kama ungekuwa na malengo madogo.
Hii ina maana kwamba kuwa na malengo madogo ni kujipotezea muda na kujizuia kukua.
Utahangaika na kuchoka, lakini matokeo utakayoyapata ni madogo sana.
Kwa kuwa na malengo makubwa, utajisukuma zaidi ya ulivyozoea, utafikia uwezo mkubwa ulio ndani yao na hapo utaweza kufanya makubwa zaidi.
Jamii inakuhadaa usiwe na malengo makubwa. Inakufanya ujisikie vizuri kwa kuhangaika na mambo madogo madogo.
Lakini matokeo yake ni kutengeneza maisha magumu.
Unajikuta ukihangaika sana lakini bado hupati matokeo ya tofauti.
Unachohitaji ni kuanza kufikiri kwa ukubwa kuliko ulivyozoea.
Kujiwekea malengo makubwa zaidi ya ulivyozoea.
Kuyaamini malengo hayo na kuyafanyia kazi bila kuchoka.
Na hapo unakuwa umejiweka kwenye nafasi ya kufanya makubwa zaidi ya ambavyo umekuwa unafanya.
Hatua ya kuchukua;
Malengo yoyote unayofanyia kazi sasa, unapaswa kuyakuza zaidi. Anza kwa kufikiri kwa ukubwa, tengeneza taswira mpya utakayoifanyia kazi na hayo yakusukume kufanya kwa utofauti na ulivyozoea.
Unaweza kuwa na ndoto kubwa, lakini malengo uliyonayo yakakukwamisha kuzifikia.
Ni wakati sasa wa kuyapitia malengo yako na kuyakuza kwa namna ambayo yataendana na ndoto kubwa ulizonazo ili kuzifikia.
Tafakari;
Kutaka kujisikia vizuri ndiyo chanzo cha maisha magumu kwa wengi.
Wengi huona hawahitaji kuwa na malengo makubwa kwa sababu hawataki kujitesa.
Lakini kinachotokea ni wanatengeneza maisha ambayo yanawatesa sana.
Chagua kuteswa na malengo makubwa ili kuwa na maisha mazuri au kuwa na malengo yasiyokusumbua ila kuwa na maisha ya mateso.
Mateso hayakwepeki.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining