#SheriaYaLeo (196/366); Tengeneza hali ya mshangao.
Watoto huwa wana tabia ya kufanya tofauti na kile tunachowaambia wafanye.
Lakini kuna hali ambazo watoto huwa wanakuwa tayari kufuata kile wanachoambiwa; pale wanapoahidiwa kitu cha kushangaza.
Inaweza kuwa ni zawadi iliyo ndani ya boksi au mchezo ambao mwisho wake hauonekani au safari ambayo mwisho wake haujulikani.
Katika hali hizo ambapo wanasubiria mshangao, wanakuwa rahisi sana kushawishika. Wanakuwa tayari kufuata chochote unachowaambia.
Tabia hiyo ya watoto bado ipo ndani ya kila mmoja wetu na ndiyo chanzo kikuu cha raha kwa wengi.
Kuongozwa na watu ambao wanajua wapi wanaenda ambapo sisi hatujui.
Ili kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine, unapaswa kutengeneza hali hiyo ya mshangazo.
Watu wasiwe na uhahika nini kinakwenda kutokea.
Hali hiyo ya kukosa uhakika ndiyo inawafanya wakufuatilie kwa karibu na hivyo kuwa tayari kushawishika.
Hupaswi kuwa mtu unayetabirika.
Maana pale watu wakishaweza kukutabiri, wakiwa na uhakika ni matokeo gani yanakwenda kupatikana, hawawi na chochote cha kuwavutia kukufuatilia kwa karibu.
Na hilo linapunguza sana ushawishi unaokuwa nao kwa watu hao.
Watu huwa wanapenda kushangazwa na huo ndiyo ufunguo wa kuwanasa na kuwashawishi kwenye kile unachotaka.
Kuwa na mwenendo ambao unawafanya watu wabaki wakijiuliza nini kinachofuata bila ya kuwa na uhakika.
Kufanya kitu ambacho hawakutegemea ufanye inawapa shauku ya kuendelea kukufuatilia kwa karibu.
Mara zote unakuwa mbele yao huku ukiwa na udhibiti mkubwa.
Hilo linawafanya wakufuatilie kwa karibu na washawishike zaidi na wewe.
Sheria ya leo; Kuna njia mbalimbali za kutengeneza hali ya mshangao; kutuma ujumbe ambao haukutegemewa, kutokea wakati ambao hukutegemewa au kuwapeleka mahali ambapo hawajawahi kwenda. Njia bora kabisa ya kuwashangaza watu ni kuonyesha kitu kipya kuhusu wewe ambacho hawakuwa wanakijua.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji