2693; Haiwezekani kwa sababu hujafanya.
Wakati Wright Brothers wanahangaika kufanya majaribio ya kurusha ndege, wanasayansi wakubwa walisema wazi kwamba binadamu hawataweza kutusha ndege kwa miaka 100 ijayo.
Kanuni zote za kisayansi zilionyesha hicho ni kitu kisichowezekana.
Lakini mwaka mmoja baadaye Wright Brothers walirusha ndege yao na mengine yakabaki historia.
Kabla ya Roger Bannister kuvunja rekodi kwa kukimbia maili moja chini ya dakika nne, ilikubalika ni kitu ambacho binadamu hawezi kufanya. Na kwamba mtu akijaribu kukimbia kwa kasi hivyo basi atakufa kabisa.
Lakini baada ya Bannister kuvunja rekodi hiyo, mwaka mmoja baadaye zaidi ya watu 30 waliweza kuivunja kabisa.
Na leo hii ni kitu cha kawaida.
Huenda kuna mambo unajiambia huwezi au haiwezekani.
Huo siyo ukweli, siyo kwamba huwezi au haiwezekani, bali ni hujawahi kufanya au kuona ikifanywa.
Hivyo basi, ukiondoa dhana ya huwezi au haiwezekani kwenye akili yako na ukafanya ukiamini itawezekana, kwa hakika itawezekana.
Huhitaji hata kujua itawezekanaje wakati unaanza, unachohitaji ni kufanya ukiamini inawezekana.
Hatua ya kuchukua;
Jiwekee lengo kubwa na ambalo unaona haliwezekani. Kisha amini sana kwenye lengo hilo na chukua hatua bila ya wasiwasi wowote.
Kila unapojiambia huwezi au haiwezekani, jikumbushe Elon Musk anapambana kwenda sayari ya Mars huko. Kila mtu anamwambia haiwezekani, lakini hawasikilizi, yeye anaendelea na mipango yake.
Nini unapambana nacho bila kujali kama inawezekana au la?
Tafakari;
Kama binadamu tungekuwa tunafanya yale tu yanayowezekana na ambayo tuna uhakika nayo, leo hii kusingekuwa na maendeleo ambayo tunayo.
Maendeleo yoyote tunayoyaona duniani leo ni matokeo ya wabishi wachache waliokataa neno haiwezekani.
Je wewe utakuwa mmoja wa wabishi hao wachache wanaoisukuma dunia?
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining