2694; Ukiwa njia panda, chagua njia ngumu.

Mara kwa mara huwa tunajikuta njia panda, tukiwa na machaguo mengi na hatujui tuchague lipi.

Hapa ndipo wengi huwa wanakwama kwa kushindwa kujua kipi sahihi kwao kuchagua.
Wanatumia muda mrefu kuchambua mambo bila kuchagua.

Na hata pale wanapofikia hatua ya kuchagua basi hukimbilia kuchagua kilicho rahisi zaidi.
Na mara nyingi hayo huishia kuwa machaguo mabovu.

Pale unapojikuta njia panda, usikubali kupoteza muda wako mwingi hila kuchagua.
Badala yake chagua haraka na chagua kile kilicho kigumu zaidi.

Kuchagua kigumu kuna manufaa makubwa mawili;
Moja ni wachache wanaochagua kigumu, hivyo ushindani unakuwa mdogo.
Mbili ni kigumu kinakusukuma kuwa bora zaidi, kinakutaka ujisukume zaidi na hivyo kutumia uwezo wako zaidi.

Jamii inakuhadaa ukimbilie mambo rahisi, inakuonyesha kila njia ya kufanikiwa bila ya kuteseka.
Lakini hebu waangalie wote ambao wanahangaika na njia hizo za jamii wamefika wapi?

Usihangaike na majaribio ambayo wote walioyafanya wameshindwa.
Wewe nenda kwenye vitu vya uhakika na vitakuwezesha kufanya makubwa.

Hatua ya kuchukua;
Kuanzia sasa, pale unapojikuta njia panda na hujui nini ufanye, jiulize kipi kigumu zaidi kwenye vile vilivyo mbele yako kisha fanya hicho.
Usihangaike na vitu rahisi, vitakupotezea muda wako bure.

Tafakari;
Siri iliyo wazi kabisa ya mafanikio ni kutokufanya yale ambayo hawajafanikiwa wanapenda kufanya.
Na kubwa kabisa ni kupenda vitu rahisi.
Ukiachana na vitu rahisi na kupenda vitu vigumu, ni lazima utafanya makubwa kwa sababu hutakutana na ushindani mkubwa na utalazimika kutumia uwezo wako zaidi.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining