#SheriaYaLeo (198/366); Ingia kwenye nafsi zao.

Ni tabia yetu sisi binadamu kujipenda na kujikubali sisi wenyewe zaidi ya wengine.
Hali hiyo ilianza tangu utotoni ambapo tulionyesha hilo wazi.

Kadiri ambavyo tumekua, hali hiyo imebaki kuwa ya ndani zaidi japo wengi hawaionyeshi kwa nje.
Tunakubali fikra na mitazamo yetu na kuona ndiyo sahihi kuliko ya wengine.

Hilo linatoa fursa kubwa ya kuweza kuwa na ushawishi kwa wengine.
Kwani unachohitaji kufanya ni kuingia ndani ya nafsi ya mtu, kuwa kama walivyo wao.

Kwa kuwa watu wanajipenda na kujikubali wao wenyewe, pale unapokuwa kama wao wanakupenda na kukukubali pia.

Unapokuwa na mtazamo, fikra, maoni na mapenzi kama yao, wanakuona wewe ni kama wao na hivyo kukukubali zaidi.

Na hilo ni rahisi sana kufanya, unapokuwa na mtu, weka umakini wako wote kwake na nenda kama anavyoenda yeye.

Mfanye ajione ni kama anajiangalia kwenye kioo. Kwa njia hiyo atashawishika zaidi na kile unachomwambia kwa sababu hawezi kujipinga yeye mwenyewe.

Sheria ya leo; Waondoe watu kwenye hali yao ya ubishi kwa kuingia kwenye nafsi zao. Unapoingia kwenye nafsi zao, wanakuona wewe kama wao na hivyo kushawishika zaidi na wewe.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji