2695; Malengo madogo ndiyo yanayokuchelewesha.
Rafiki, watu huwa wanadhani kwamba ukiweka malengo makubwa halafu usiyafikie basi umeshindwa.
Hiyo siyo kweli, ukiweka malengo makubwa kabisa na usiyafikie, bado wewe ni mshindi.
Kwa sababu utakachokuwa umepata siyo sawa na ambacho ungepata kama usingekuwa umeweka malengo hayo makubwa.
Kushindwa ni pale unapoweka malengo madogo halafu ukayafikia.
Hapo ni kushindwa kwa sababu unafanya kile ulichozoea, hakuna namna unajisukuma kwa ukubwa zaidi.
Ukiweka malengo madogo na ukayafikia unajisikia vizuri, wakati hakuna hatua yoyote kubwa.
Unapojisikia vizuri unaona kama umemaliza kila kitu, wakati bado sana.
Ndiyo maana nakuambia malengo madogo ndiyo yanayokuchelewesha kwenye safari yako ya mafanikio.
Unajiwekea malengo yanayokufurahisha na ukiyafikia unafurahi na kujiona upo pazuri.
Unapaswa kujiwekea malengo ambayo yanakutisha, ambayo yanakupa wasiwasi na hayakufanyi ujisikie vizuri.
Ni malengo hayo ndiyo yatakayokusukuma ufanye zaidi ya ulivyozoea, upambane kweli kweli.
Na hata kama hutayafikia malengo hayo, bado hatua utakazokuwa umepiga ni kubwa kuliko ambazo ungepiga kwa malengo yako madogo.
Lakini swala la utayafikia au hutayafikia malengo halipaswi kukusumbua.
Wewe unachohitaji ni malengo makubwa na kupambana nayo kwa kila namna.
Chukua mfano umekuwa unauza laki moja kila wiki.
Ukijiwekea lengo la laki moja na ukalifikia, utajisikia vizuri, lakini je nini kimebadilika? Hakuna, uko vile vile na uko pale pale.
Vipi kama ukiweka lengo jipya la mauzo la milioni kwa wiki. Ah, hilo kwanza litakushtua, hujawahi kufikiri hivyo. Utaanza kwa kujiambia hakuna namna unaweza kufikia.
Na hapo hupaswi kuhangaika na kama utalifikia au la, bali unapaswa kuweka mkakati wa kulifikia na kuufanyia kazi.
Hata kama hutafikia lengo hilo la milioni, hata ukifikia laki 5, bado ni kubwa sana kuliko laki moja uliyokuwa umezoea.
Naamini umeipata picha hapo.
Lakini sasa usijiambie hutafikia lengo, amini bila ya shaka yoyote ile kwamba utaweka juhudi kubwa mpaka ulifikie lengo.
Amua hakuna kingine kitakachokusumbua isipokuwa lengo lako kubwa.
Na utayaona maajabu makubwa kwenye maisha yako.
Hatua ya kuchukua;
Unapaswa kuwa na lengo moja kubwa sana ambalo linakutisha, lakini unaliamini na kulifanyia kazi.
Siyo lengo la mbali, yaani ndoto za baadaye, bali lengo unalofanyia kazi sasa.
Na mahali pazuri pa kujiwekea lengo hilo ni kwenye mauzo.
Jipe namba kubwa ya mauzo ambayo unapaswa kuifikia.
Kisha jisukume kwa kila namna kufikia namba hiyo.
Jua huwezi kushindwa kwenye lengo hilo kubwa, kwa vyovyote vile, utapata ushindi.
Tafakari;
Watu hawashindwi kwenye maisha kwa sababu wanajaribu makubwa na kuanguka.
Bali watu wanashindwa kwenye maisha kwa sababu wanajaribu madogo na kuyafanikisha.
Chochote kinachokufanya ujisikie vizuri kinafanya maisha yako yawe mabaya.
Na chochote kinachokufanya ujisikie vibaya kinafanya maisha yako yawe magumu.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining