2701; Bila msimamo umefika hapo, vipi ukiweka msimamo?

Pamoja na kukosa msimamo mkubwa kwenye yale unayofanya, umeweza kufika hapo ulipo sasa.

Umekuwa hufanyi mambo kwa viwango vya juu kabisa mara zote.
Kuna wakati unahamasika na kufanya kwa viwango vya juu.
Na kuna wakati mazoea yanakuingia na unafanya kwa mazoea.

Pamoja na hayo, bado umeweza kupiga hatua ambazo umepiga mpaka sasa. Hata kama siyo kubwa, kitendo cha kuendelea kuwepo, ni ushindi mkubwa.

Sasa hebu pata picha ni matokeo ya aina gani utayapata pale utakapoanza kufanya kwa msimamo mara zote bila kuacha?
Fikiria pale utakapoweza kufanya kwa viwango vya juu mara zote bila kuruhusu mazoea ya aina yoyote ile.

Hakuna ubishi, lazima utapata matokeo makubwa kuliko unayoyapata sasa.

Sasa je ni nini kinakuzuia usifanye kwa msimamo?
Amua leo kujiwekea viwango vyako vya ufanyaji na kwenda navyo kwa msimamo.
Chagua mambo ambayo utayafanya kila siku bila ya kujali nini kinaendelea au matokeo gani unayoyapata.

Kwa kuwa bila hata ya msimamo mkubwa uliweza kufanya hayo uliyofikia sasa, kuongeza msimamo kutakusukuma zaidi.

Hatua ya kuchukua;
Kwenye biashara yako, weka msimamo kwenye vitu vikubwa; masoko na mauzo. Fanya hivyo viwili kila siku bila ya kuacha hata siku moja.
Halafu angalia jinsi ambavyo matokeo mazuri na makubwa yatazalishwa kwenye biashara yako.

Tafakari;
Kukosa msimamo ndiyo kikwazo kikubwa kwako kupiga hatua kubwa zaidi.
Hayo unayofanya sasa ndiyo ya msingi, ila kushindwa kuyafanya kwa msimamo ndiyo kunakukwamisha.
Weka msimamo kwenye kile unachofanya na utapata makubwa zaidi.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining