2712; Utakuja kushangazwa na matokeo.

Kitu kinachowakwamisha wengi kwenye kuendelea kuchukua hatua ni kutokuyaona matokeo haraka.

Mtu anataka kupunguza uzito, anahamasika kufanya mazoezi.
Anaanza mazoezi kwa siku chache, ila kila akipima uzito uko pale pale.
Anajiambia haya mazoezi hayafanyi kazi na kuamua kuachana nayo.

Mtu anataka kuongeza mauzo kwenye biashara yake, anahamasika kuwapigia simu na kuwatembelea wateja, wengi wanamwahidi watakuja kununua, lakini bado mauzo yanabaki pale pale.
Anajiambia hayo mambo hayafanyi kazi, hivyo anaachana nayo.

Hivyo ndivyo wengi wamekuwa wakienda kwa maisha yao yote na ndiyo maana mafanikio yanakuwa magumu.

Huwezi kufanikiwa kwa kutegemea matokeo ya hapo kwa hapo.
Huwezi kufanikiwa kwa kuanza vitu na kuishia njiani.

Kama kitu ni muhimu, unachopaswa ni kukifanya kila siku bila kuacha, hata kama huoni matokeo.
Utakuwa pazuri zaidi kama utaendelea kufanya bila ya kuangalia matokeo.

Wajibu wako wewe ni kufanya, kama ulivyopanga kufanya.
Na matokeo yanakujaje hilo lisikusumbue sana.

Maana hata ukiacha kufanya kwa sababu huoni matokeo, huo muda hautasimama, utamezwa na mambo mengine, tena mambo yasiyokuwa na tija kabisa.

Chagua kufanya bila ya kuhangaishwa na matokeo, hasa mwanzoni.
Na baadaye matokeo yatakuja kukushangaza sana.
Kwani yatakuja kwa ukubwa mno na kwa wakati mmoja.
Mpaka utajiuliza haya matokeo yalikuwa yamejificha wapi.

Hatua ya kuchukua;
Jua kile kilicho sahihi kwako kufanya kisha kifanye kama ulivyopanga bila ya kuacha kwa sababu ya matokeo hafifu unayopata.
Wajibu wako ni kufanya, matokeo achana nayo.

Tafakari;
Kufanya na matokeo huwa haviambatani pamoja.
Weka juhudi kubwa kwenye kufanya maana ndiyo kilicho ndani ya uwezo wako.
Matokeo yapo nje ya uwezo wako, usihangaike nayo sana.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining