2716; Nataka nikuoe/unioe.

Pata picha, umekutana na mtu mahali kwa mara ya kwanza, humjui hakujui na hapo hapo akakuambia anataka akuoe/umuoe.

Ni jambo ambalo litakushtua na kukushangaza.
Iweje mtu akutake ufanye maamuzi makubwa hivyo wakati hata bado hamjajuana?

Maamuzi ya kuoa/kuolewa na mtu huwa yanajengeka taratibu baada ya watu kuwa na ukaribu wa muda mrefu.
Kupitia urafiki na uchumba ndiyo watu mnajuana na kushawishika kama mnaweza kwenda pamoja.

Hii makala haihusu uchumba wala kuoana, bali inahusu masoko na mauzo.

Tumekuwa tunashindwa kuuza zaidi kwenye biashara zetu kwa sababu tumekuwa tunataka wateja wanaotujua kwa mara ya kwanza wanunue hapo hapo.

Tunataka watu wafanye maamuzi makubwa ya kutengana na fedha zao na kutupa, wakati hawajui chochote kuhusu sisi.

Hiyo haina tofauti na kutaka mtu akuoe/aolewe na wewe siku ya kwanza mnapojuana.

Kutengeneza wateja kwenye biashara ni mchakato kama ilivyo kwenye uchumba na kuoana.
Lazima mjuane kwanza, muaminiane ndipo hatua nyingine ziendelee.

Hapo ndipo masoko yanapoingia kwenye biashara.
Lengo la masoko ni kujenga mahusiano mazuri na wateja wako tarajiwa ili wawe tayari kununua kile unachouza.

Masoko yanakuwezesha kujenga imani kwa wateja na kuwaonyesha manufaa makubwa wanayokwenda kupata kwa kununua kile unachouza.

Wanapokutana na wewe au biashara yako kwa mara ya kwanza hawaambiwi kuhusu kununua, bali wanaonjeshwa kwanza manufaa yaliyopo.

Ni kupitia kuonja manufaa hayo ndiyo wanashawishika kupata zaidi na hapo wanakuwa tayari kununua.

Njia hiyo ni ya uhakika na yenye nguvu kuliko kuwalazimisha wateja wanunue mara ya kwanza wanapokujua.

Hatua ya kuchukua;
Tengeneza mchakato wa uchumba kwenye biashara yako. Pale unapomfikia mteja tarajiwa kwa mara ya kwanza, usimlazimishe kununua, badala yake mwonyeshe manufaa anayokwenda kuyapata, nasa hisia zake na yeye mwenyewe atasukumwa kununua.
Hili linahitaji uweke kazi zaidi, lakini lina manufaa makubwa kuliko kulazimisha watu kununua.

Tafakari;
Hakuna anayependa kuuziwa, bali kila mtu anapenda kununua vitu ambavyo vina manufaa kwao.
Lengo lako kama muuzaji siyo kuwauzia watu, bali kuwasaidia katika kununua.
Waonyeshe manufaa wanayokwenda kuyapata na watashawishika wao wenyewe kununua kile unachouza.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining