2717; Nusu muda, muda kamili na muda wote (au safari ya kuelekea kwenye ubilionea).
Siku chache zilizopita nilikuwa naangalia video kwenye mtandao wa youtube.
Nilikutana na video moja ya Patrick Bet David ambapo alikuwa anaelezea hatua nne za kupata utajiri mkubwa.
Kitu kipya nilichojifunza kwenye video hiyo ni dhana ya muda ambao mtu anaweka kwenye safari hiyo ya utajiri.
Amegawa muda huo kwenye makundi matatu ambayo ni;
Nusu muda (part time)
Muda kamili (full time)
Na muda wote (all time)
Hoja yake kuu ikiwa ni kwamba ili upate mafanikio makubwa na yanayodumu, unapaswa kuwa mtu wa muda wote (full timer).
Huwezi kupata mafanikio makubwa kwa kuwa mtu wa kufanya kazi nusu muda (part timer) au muda kamili (full timer).
Kuna maeneo manne muhimu aliyogusia na viwango vya muda kwemye makundi hayo matatu.
Eneo la kwanza ni nidhamu ya kazi.
Kazi inahitajika sana katika safari ya mafanikio.
Kipimo cha kazi ni muda ambao mtu anatumia kwenye kuweka juhudi na siyo muda ambao mtu anakuwa eneo la kazi.
Kufanya kazi masaa 40 kwa wiki hiyo ni nusu muda.
Kufanya kazi masaa 60 kwa wiki ni muda kamili.
Kufanya kazi masaa 80 kwa wiki ndiyo muda wote.
Hivyo ili upate mafanikio na utajiri mkubwa, ni lazima ufanye kazi muda usiopungua masaa 80 kwa wiki.
Na huo ni muda unaoweka juhudi, siyo muda unaokuwa eneo la kazi ukiupoteza kwa mambo yasiyo na tija.
Eneo la pili ni kasi ya ukuaji binafsi.
Pamoja na kuweka juhudi kubwa kwenye kazi, lazima uwe na ukuaji binafsi.
Maana huwezi kupata matokeo ya tofauti kama wewe mwenyewe hukui.
Ukuaji binafsi unatokana na uwekezaji unaofanya ndani yako kupitia kujifunza kwa usomaji wa vitabu.
Hapa pia kuna vipimo vitatu kwenye kasi ya ukuaji binafsi.
Kusoma vitabu viwili kwa mwezi ni nusu muda.
Kusoma vitabu vinne kwa mwezi ni muda kamili.
Kusoma vitabu nane kwa mwezi ni muda wote.
Ili upate mafanikio makubwa na utajiri ni lazima uwe mtu wa kujifunza muda wote.
Kwa wiki usome vitabu visivyopungua viwili, ambapo kwa mwezi vitakuwa vitabu nane na kwa mwaka vitabu 100.
Eneo la tatu ni vikwazo kwenye safari.
Safari ya mafanikio huwa haijanyooka, huwa kuna vikwazo vya kila aina.
Vikwazo vinawafanya wengi kukwama au kuacha na baadaye kurudi tena.
Hapa kwenye vikwazo pia kuna vipimo vitatu;
Anayepata vikwazo viwili mpaka vinne kwa mwaka anaweka nusu muda.
Anayepata kikwazo kimoja ndani ya mwaka anaweka muda kamili.
Anayepata kikwazo kimoja ndani ya miaka 5 mpaka 10 anaweka muda kamili.
Ili upate mafanikio na utajiri mkubwa, hupaswi kuruhusu vikwazo mbalimbali unavyokutana navyo vikuzuie kuendelea na safari yako.
Kadiri unavyokatishwa na vikwazo, ndivyo unavyojichelewesha kufanikiwa.
Eneo la nne ni aina ya biashara ambazo mtu anafanya.
Kubadili aina ya biashara ambayo mtu unafanya huwa ni kikwazo sana kwa mtu kufikia utajiri na mafanikio makubwa.
Hapa kuna vipimo vitatu.
Wanaobadili biashara kila baada ya mwaka mmoja mpaka miwili ni nusu muda.
Wanaobadili biashara kila baada ya miaka 5 mpaka 10 ni muda kamili.
Wanaobadili biashara kila baada ya miaka 20 mpaka 40 ni muda wote.
Ili kupata mafanikio makubwa, lazima ukae kwenye biashara moja kwa muda mrefu.
Kuhangaika na biashara mpya kila wakati ni kujizuia kupata mafanikio makubwa.
Mengineyo.
Patrick alimalizia na mengineyo muhimu katika hii safari kama;
Mafanikio inabidi yawe lazima kwako na siyo tu kitu cha kutamani.
Lazima uweke umakini mkubwa.
Uwe na ndoto kubwa.
Uwe na shauku ya kufikia ndoto hizo.
Ujiweke kwenye nafasi nzuri ya kupata unachotaka.
Ujenge mali inayokua thamani.
Uoe/kuolewa na mtu sahihi.
Uwe na hasira ya kufanikiwa.
Uwe na adui unayepambana naye kumshinda.
Uchukue hatua za hatari.
Utoe thamani kubwa.
Uweze kufanya maamuzi sahihi.
Uwe na marafiki sahihi.
Ujiweke kwenye nafasi ya kupata bahati.
Ukubali kuonekana kichaa na uliyechanganyikiwa.
Hatua ya kuchukua;
Jipime kwenye maeneo manne muhimu na jua kama upo kwenye nusu muda, muda kamili au muda wote.
Unajua unakopaswa kuwa, kama unataka mafanikio makubwa, jiweke kwenye muda wote.
Hilo lipo ndani ya uwezo wako, ni wewe kulifanyia kazi.
Tafakari;
Mafanikio siyo kitu cha nusu muda au muda kamili, bali ni kitu cha muda wote.
Wengi hawafanikiwi kwa sababu hawawezi muda wao mwingi kwenye kile kinachoweza kuwapa mafanikio.
Badala yake wanatawanya muda huo kwenye mambo mengi yasiyo na tija.
Wewe usiwe hivyo, weka muda wako wote kwenye safari ya mafanikio na utayapata mafanikio makubwa.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining