2718; Nidhamu ya kazi.

Kwenye ukurasa uliopita tumejifunza kuhusu mambo manne ya kufanyia kazi ili kupata mafanikio makubwa.

Moja ya mambo hayo ni nidhamu ya kazi.
Tumeona ni lazima uweke kazi ya kutosha ndiyo uweze kupata matokeo makubwa unayoyataka.

Kutoka kwa mwandishi yule yule, Patrick Bet David tunajifunza mambo ya kuzingatia kwenye kujijengea nidhamu ya kazi.

  1. Kuwa unayetabirika.
    Wafanye watu waweze kukutegemea na kuwa na uhakika na wewe kwamba unakwenda kufanya kilicho sahihi na bora muda wote.

  2. Kuwa na msimamo.
    Panga na kufanya kama ulivyopanga bila kuacha. Wewe fanya hata kama huyaoni matokeo.

  3. Kuwa na maandalizi.
    Panga nini unakwenda kufanya na jiandae mapema ili uweze kufanya kama ulivyopanga.

  4. Fanya zaidi.
    Kwa chochote unachofanya, nenda hatua ya ziada kwa kufanya zaidi ya ulivyozoea au ilivyozoeleka.

  5. Kuwa na mtazamo wa kufanya sasa.
    Chochote unachopanga kufanya, anza kukifanya mara moja. Hiyo ndiyo tiba ya kuahirisha kambo.

  6. Ongozana na watu sahihi.
    Ambatana na watu wanaoweka kazi kweli, wanaotaka kufika mbali zaidi.

  7. Fanya kazi kwa nguvu na akili.
    Kuna watu watakuambia usifanye kazi kwa nguvu, bali fanya kwa akili.
    Hawajui wanalosema, wewe fanya kazi kwa nguvu na kwa akili.

  8. Ondokana na usumbufu.
    Usumbufu ni mwingi ambao unawinda umakini wako.
    Kata kila aina ya usumbufu ili utumie muda wako kwa yale yenye tija.

  9. Weka umakini wako wote kwenye kazi.
    Usifanye kazi huku mawazo yako yapo kwenye kitu kingine.
    Weka umakini wako wote kwenye kile unachofanya.

  10. Kuwa na orodha ya vitu vya kufanya.
    Usiianze siku bila ya kuorodhesha vitu unavyokwenda kufanya (TO DO LIST). Na ukishaorodhesha vya kufanya, usitoke nje ya orodha yako.

  11. Kula kwa usahihi.
    Unachokula kina athari kwenye mwili na nguvu zako hivyo kuathiri sana ufanyaji wako wa kazi.
    Kula vyakula sahihi vinavyokupa nguvu ya kuweza kuweka juhudi kwenye kazi.
    Epuka vyakula vinavyouchosha mwili na kupunguza kasi yako ya kazi.

  12. Ziba matundu yanayovuja.
    Kuna vitu unafanya ambavyo vinapoteza muda ambao ungeweza kuutumia kwenye kazi.
    Acha kufanya vitu hivyo mara moja ili uweze kupata muda mwingi wa kuweka kwenye kazi.

  13. Punguza mambo unayofanya.
    Kanuni ya pareto, asilimia 80 ya matokeo yanazalishwa na asilimia 20 ya juhudi unazoweka.
    Weka juhudi zako kwenye mambo machache yenye matokeo makubwa.

  14. Achana na ukamilifu.
    Usisubiri mpaka uwe mkamilifu ndiyo ufanye kitu. Anza kufanya na utaendelea kukamilisha kadiri unavyokwenda.

  15. Epuka uchovu uliopitiliza kwa kuwa na pa kutorokea.
    Kuna kitu unapenda kufanya ambacho hakihusishi kazi. Kitumie hicho kama sehemu ya kutorokea ili usipate uchovu uliopitiliza na kushindwa kuendelea kuweka juhudi kubwa kwenye kazi.
    Baada ya kuweka juhudi kubwa kwenye kazi, fanya kile unachopenda kufanya. Kwa namna hiyo utaepuka kuchoka kupitiliza.

Hatua ya kuchukua;
Imarisha nidhamu yako ya kazi kwa kufanyia kazi haya uliyojifunza hapa leo.

Tafakari;
Kazi ndiye rafiki wa kweli ambaye hawezi kukutupa kwa namna yoyote ile.
Jenga urafiki na kazi, jijengee nidhamu bora kabisa ya kazi na hakuna kitakachokushinda kwenye maisha.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining