2720; Unataka au hutaki?

Hadithi tulizokuwa tunajifunza utotoni zilikuwa na mafunzo makubwa sana, japo siyo mara zote tuliweza kuyang’amua.

Chukua mfano wa hadithi ya sungura na ndizi.
Sungura anapita zake, anaziona ndizi, anaona ni nzuri na kujiambia anazitaka.

Anaanza kurukia ndizi zile.
Anaruka na kuruka tena,
Lakini hazifikii ndizi.
Anaruka zaidi na zaidi lakini wapi.
Mwisho anajiambia, hata hivyo ndizi zenyewe ni mbichi, sizitaki mbichi hizo.

Rafiki, hakuna mtu ambaye amewahi kukosa kile kweli anachokitaka.
Na hakuna mtu amewahi kukosa sababu ya kutokupata kile ambacho hakitaki kweli.

Yaani, kama kuna kitu unakitaka kweli na hakuna namna unaweza kukubali kutokukipata, basi utakipata.
Dunia itafanya kila njama mpaka ihakikishe umepata kile unachotaka.

Na kama kuna kitu hukitaki kweli, utakuwa na sababu nyingi na zinazoonekana zenye mashiko kabisa kwa nini huhitaji kukipata.

Ninachotaka tujikumbushe hapa ni kupata au kukosa kitu kunaanza na sisi wenyewe.
Unakitaka kitu kiasi gani na umejitoa kiasi gani kukipata ndiyo itaamua kama utakipata au la.

Hivyo ni vyema tukaacha kujidanganya kwa kutumia sababu mbalimbali.
Tuwe wakweli kwetu wenyewe.
Kama kweli tunakitaka kitu tuwe tayari kufanya kila namna kukipata na tusikubali kuishia njiani.

Na kama kweli hatukitaki kitu, kama tunaona hakina thamani ya sisi kuhangaika nacho pia tujiambie wazi hatukitaki kabla hata hatujaanza kuhangaika nacho.

Hakuna kitu kinaumiza kama kuweka juhudi nusu kwenye kitu ambacho hukitaki kweli halafu ukaishia njiani kwa kujiambia hakifai.
Maana juhudi hizo unakuwa umezipoteza bure.

Fikiria kama sungura angejiambia mapema ndizi ni mbichi, asingepoteza muda na nguvu kuanza kuzirukia.
Angetunza muda na nguvu hizo kwa mambo mengine muhimu kwake.

Hicho ndiyo kikubwa cha kuondoka nacho hapa.
Kama unakitaka kitu kweli, kipambanie mpaka kukipata.
Na kama haupo tayari kupambania kitu mpaka kukipata, usijaribu hata kukianza, ni kupoteza tu bure.

Hatua ya kuchukua;
Ni nini ambacho unakitaka kweli kwenye maisha yako na uko tayari kukipambania mpaka kukipata bila ya kukata tamaa?
Kiandike hicho leo na kila siku na kipambanie mpaka ukipate.
Kila unapokaribia kukata tamaa kwa sababu unaona huwezi kukipata, jikumbushe kwa nini ulikianza na uwekezaji mkubwa ambao tayari umeshaufanya hapo.
Usikubali kupoteza kila kitu.

Tafakari;
Kila mtu kwenye maisha huwa anapata kile anachokitaka hasa, kile ambacho yupo tayari kukivumilia.
Upo hapo ulipo sasa kwa sababu umekuwa tayari kupavumilia.
Ukiendelea kupavumilia utaendelea kubaki hapo.
Ukishindwa kupavumilia utakwenda pengine tofauti na hapo.
Yote hayo yanaanzia ndani yako na yanakutegemea wewe zaidi.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining