2722; Wanadanganya, lakini tunawakubali.

Umewahi kuangalia maigizo au tamthilia mbalimbali.
Na katika hizo, kuna ambazo zilinasa hisia zako, ukajikuta ukifurahi na kucheka au kuhuzunika na kulia.

Ulijua kabisa kila kilichokuwa kinaonyeshwa kwenye maigizo au tamthilia siyo ukweli. Kama ni mtu amekufa kwenye igizo au tamthilia unajua kabisa kwamba hajafa kweli.
Ameigiz tu kufa.
Lakini bado ulihuzunika na hata wakati mwingine kutokwa machozi.

Pamoja na kujua kwa mantiki kwamba kilichopo kwenye maigizo na tamthilia siyo kweli, bado hisia zetu huwa zinanaswa kama vile ni kitu cha kweli.
Na hisia zikishanaswa, hatuna tena ujanja.

Kuna funzo kubwa sana hapa kwa ajili yetu.
Kwamba kilicho muhimu na chenye nguvu kwetu siyo namna tunavyofikiri, bali namna tunavyohisi.
Hisia zina nguvu kubwa kwetu kwenye kufanya maamuzi.

Hivyo katika kuwashawishi watu, usiangalie fikra pekee, badala yake angalia na hisia pia.
Angalia ni kwa namna gani unaweza kugusa hisia zao na hilo kuwasukuma kukubaliana na wewe.

Hisia kuu ya kugusa ni kuwafanya watu wajisikie vizuri.
Unapowafanya watu wajisikie vizuri kwa uwepo wako, watashawishika na kukubaliana na wewe.

Kwa maana hiyo basi, kila kitu kwenye maisha ni kuigiza.
Unapaswa kuigiza kwa namna ambayo utawafanya watu wajisikie vizuri kupitia uwepo wako.
Hilo litawavuta zaidi kwako na watashawishika na wewe.

Na sehemu muhimu ya kutumia hili ni kwenye mauzo.
Unapotaka kuwashawishi watu wanunue kile unachouza, hatua ya kwanza na muhimu ni kuwafanya wakukubali kwanza.
Na ili wakukubali, lazima uwafanye wajisikie vizuri.

Hapo ndipo maigizo mbalimbali yanapohitajika, kuanzia kwenye mwonekano, mavazi na hata namna unavyoongea.
Yote yanapaswa kupangiliwa kwa namna itakayomfanya mteja ajisikie vizuri, akukubali na kuwa tayari kununua unachouza.

Huigizi ili kudanganya,
Bali unaigiza ili kumsaidia mtu akubali kile chenye manufaa kwake.
Na mara zote watu huwa wanasahau mambo mengi, ila huwa hawasahau hisia walizopata kwenye kitu fulani.

Gusa hisia za watu kwa namna bora na utakuwa na ushawishi kwao ambao una manufaa makubwa na unadumu kwa muda mrefu.

Hatua ya kuchukua;
Lipi igizo lako kuu kwenye mauzo unalotumia ili kuwashawishi wateja?
Kama huna igizo ni wakati sasa wa kulitengeneza ili uweze kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine.

Tafakari;
Kila mtu duniani anaigiza.
Wale wanaopata mafanikio makubwa ni wanaoweza kuigiza kwa namna bora na kukamata hisia za watu wengi.
Tengeneza igizo lako ambalo linanasa hisia za wengi na kuwashawishi wakubaliane na wewe.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining