#SheriaYaLeo (226/366); Penyeza kwenye akili zao.

Ili uweze kuwa na ushawishi kwa watu, lazima kwanza uweze kupenyeza kwenye akili zao.

Mara nyingi watu ambao wana madaraka makubwa huwa hawapo tayari kusikiliza ushauri, hasa wa walio chini yao.
Huku wale wasio na madaraka wakiona hawahitaji ushauri huo.

Ili kuvuka ukinzani huo, unapaswa kupenyeza akili za watu kwa kutumia maandiko ambayo yana sifa tatu.

Moja ni kuwa na ushauri wenye manufaa kwa watu, ushauri unaowaonyesha jinsi ya kupata kile wanachokitaka sana.
Kwa kuwa sisi binadamu ni wabinafsi, huwa tunasikiliza kitu kinachogusa maslahi yetu.

Mbili ni kutumia mifano ya kihistoria ambayo inaonyesha wazi jinsi ambavyo ushauri unaotoa umekuwa unatumika tangu enzi na enzi. Hapo unatumia hadithi zinazoonyesha waliojufaika kwa kufuata ushauri huo na walioathirika kwa kuupuuza.
Watu huwa wanaelewa zaidi hadithi kuliko maelezo matupu.

Tatu ni kuwapa watu msukumo wa kuchukua hatua. Badala ya watu kusoma na kubaki walivyokuwa, maandiko yako yanapaswa kuwasukuma wachukue hatua fulani mara moja. Ni kupitia hatua wanazochukua ndiyo watu wanazidi kushawishika na kile walichojifunza.

Sheria ya leo; Maandiko ni njia bora ya kupenyeza akili za watu na kuwashawishi, lakini yanapaswa kuwasilishwa vizuri ili watu wayapokee, wayaelewe na wachukue hatua. Kuwa na mkakati sahihi katika kufikisha ujumbe wako kwa wale unaowalenga ili uweze kuwa na tija.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji