2723; Ukishapanda mbegu.
Kila mmoja hapa anajua kitu kuhusu kilimo, maana tumepita mazingira ambayo kilimo ni jambo la msingi.
Katika kilimo kuna kupanda, kupalilia na kuvuna.
Huwezi kuvuna kama hujapanda, hivyo cha msingi kabisa ni kuhakikisha unapanda.
Lakini pia unapopanda, huwezi kutegemea kuvuna hapo hapo.
Lazima ujipe muda, uwe na subira, vitu viote, uvipalilie, uweke mbolea na ndiyo mwishoni uweze kuvuna.
Sasa hebu pata picha umekutana na wakulima wa aina hii;
Anapanda mbegu na kesho yake kama hazijaona anasema haifanyi kazi, anaondoka na kwenda kufanya mengine.
Au anapanda mbegu, hazipalilii na hivyo zinamezwa na magugu.
Au anapanda mbegu, anazipalilia vizuri na kusubiri kuvuna, hapandi tena nyingine.
Kwa sifa hizo, unajua kabisa kwamba hapo umekutana na wakulima ambao hawawezi kufanikiwa.
Maana mafanikio kwenye kilimo yanahitaji subira kwenye kupanda na kusubiri mazao yaote, kuendelea kuyatunza mpaka kuyavuna.
Lakini lililo muhimu ni kuendelea kupanda, ili unapovuna yaliyotangulia, mengine yanaendelea kukomaa.
Sasa hii makala siyo kuhusu kilimo, bali biashara.
Biashara ni kama kilimo na mchakato wa kupata mteja mpya mpaka anunue ni sawa na kupanda mbegu mpaka kuvuna.
Pana mchakato katika kumshawishi mtu kutoka mteja tarajiwa mpaka kuwa mteja kamili aliyenunua.
Moja unahitaji njia ya kuwafikia wateja tarajiwa wengi ili wajue kuhusu uwepo wa biashara yako (kupanda mbegu).
Mbili unahitaji muda katika kwenda nao hao wateja mpaka wajenge imani na kununua (kupalilia mpaka kuvuna).
Tatu unahitaji kuendelea kufikia wateja wengi tarajiwa ili usikaukiwe na wateja wa kuwafanyia mchakato ili wanunue (kuendelea kupanda mbegu).
Wafanyabiashara wengi hawana machakato wa aina hii na ndiyo maana biashara zinakuwa ngumu kwao.
Wewe usikubali kuwa hivyo, jifunze sifa za mkulima bora na zitumie kwenye biashara.
Kila wakati kuwa na mbegu unazopanda, mimea unayopalilia na mazao unayovuna.
Kila wakati.
Hatua ya kuchukua;
Boresha mfumo wako wa masoko na mauzo kwenye biashara yako ili kila wakati uwe unapanda mbegu, unapalilia na kuvuna.
Hayo siyo mambo ya kufanya mara moja bali ni mambo ya kufanya kila wakati.
Tafakari;
Kama hujapanda mbegu, usitegemee kuvuna. Kama huna mkakati wa masoko endelevu kwenye biashara yako, usitegemee kupata wateja wengi wapya.
Ukishapanda mbegu, endelea kuihudumia kwa subira mpaka uweze kuvuna. Usitegemee mtu kuijua biashara yako na kununua hapo hapo, lazima ajenge imani kwanza.
Zoezi la kupanda mbegu linapaswa kuwa endelevu. Kamwe usiache kufanya masoko hata kama tayari una wateja wengi. Wateja wapya wanahitajika kila wakati kwenye biashara.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining