#SheriaYaLeo (229/366); Tumia ubishi wao kuwashawishi.
Kijana wa mfanyabiashara ya mikopo alienda kwa kiongozi wa dini akilalamika jinsi amejaribu kumshawishi baba yake azingatie misingi ya dini kama kusali lakini baba yake huyo alidai hana muda wa hayo mambo ya dini.
Kiongozi huyo wa dini alikuwa anajua tabia za baba wa kijana huyo, kwamba ni mtu bahili sana na anayependa kupata fedha zaidi. Fedha ilikuwa kipaumbele kwake na dini aliona inampotezea muda.
Hivyo kiongozi huyo alimwambia kijana akamwambie baba yake kwamba atamlipa kwa kila muda atakaofanya mambo ya dini kama maombi na mengine.
Mfanyabiashara huyo aliposikia huo mpango alifurahishwa nao sana. Aliona ni njia nzuri ya kumnyamazisha kijana wake huku akiingiza fedha pia. Kila siku akawa anasali na baada ya kumaliza alituma bili yake kwa kiongozi huyo wa dini ambaye alimlipa siku hiyo hiyo.
Alifanya hivyo kwa siku sita bila kuacha, lakini siku ya saba hakupeleka bili kwa kiongozi wa dini.
Kiongozi huyo wa dini alijua tayari imeshakuwa tabia kwake na ameshaizoea na kunufaika nayo kiasi kwamba hahitaji tena fedha.
Na kweli siku chache baadaye mfanyabiashara huyo alimweleza kiongozi wa dini kwamba hahitaji kulipwa tena kusali, kwani kusali kumekuwa na manufaa makubwa kwake.
Kijana wake alimshukuru sana kiongozi huyo wa dini na kuwa mchangiaji mkubwa kwenye hekalu lake.
Pale watu wanapokuwa wagumu na wabishi kubadilika, kutumia maneno haiwezi kusaidia kuwashawishi, kwani watazidi kusimamia upande wake.
Unachopaswa kufanya ni kujua maslahi yao yako wapi na kuyatumia hayo kuwashawishi.
Tumia maslahi ya watu kuwashawishi kubadilika.
Kwa kuwa kila mtu huwa anajali maslahi yake, anakuwa tayari kubadilika ili kunufaika zaidi.
Wakati mwingine unaweza kuwapambanisha na ubishi wao wenyewe, kuwafanya wajilazimishe wao wenyewe kubadilika ili kujipinga wao wenyewe.
Usibishane au kuhangaishana na watu unaotaka wabadilike. Tumia maslahi yao na wao wenyewe watakuwa tayari kubadilika.
Sheria ya leo; Watu huwa hawapo tayari kufanya kile wanacholazimishwa na wengine kufanya. Huwa wanataka kuonyesha kwamba wana maamuzi yao ambayo wanayasimamia. Lakini kila mtu ana maslahi binafsi ambayo anayajali sana. Kwa kujali maslahi yao na kuwaonyesha jinsi watakavyonufaika kwa kubadilika, watakuwa tayari kubadilika bila ya kutumia nguvu kubwa.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji