2726; Huhitaji kuvumbua kitu kipya.
Kama unatengeneza chombo cha mwendo, tairi inabaki kuwa tairi.
Huhitaji kuja na aina mpya ya uvumbuzi wa tairi.
Hata utengeneze tairi kwa upya kiasi gani, itabaki kuwa ya duara.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mambo mengi ya maisha yako.
Mengi unayopitia kama changamoto au mkwamo siyo ya kipekee kwako.
Bali ni mambo ambayo wengine wengi walishayapitia na wakaweza kuyatatua vizuri kabisa.
Na uzuri ni walipoyatatua hawakuficha suluhisho lao, badala yake wameliweka wazi kabisa.
Wameandika vitabu ambapo wameelezea kile walichopitia na jinsi walivyokivuka.
Wajibu wako wewe ni kufuata kile walichofanya ili na wewe uweze kuvuka kila unachopitia.
Kwa chochote unachopitia, huhitaji kuanza upya kabisa katika kukitatua.
Badala yake unapaswa kuangalia nani aliyewahi kupitia kama hicho na alikitatuaje.
Kisha iga kile walichofanya wengine ili uweze kutatua unachopitia.
Hatua ya kuchukua;
Ni kitu gani kikubwa kinachokutatiza au kukukwamisha?
Tafuta wengine ambao wamewahi kupitia hicho na kuweza kukitatua, kisha iga kile walichofanya.
Tafakari;
Hakuna kitu kipya chini ya jua.
Yote unayopitia wengine pia walishayapitia.
Na wakaweza kuyatatua vyema.
Wajibu wako ni kufanya kama wengine walivyofanya ili kuondoka pale ulipokwama.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining