2729; Lazima damu zimwagike.

Maisha ni vita ambayo mwisho wake unajulikana, ambao ni maisha yatashinda na wewe kuanguka. Hilo ni swala la muda tu.

Lakini kabla ya matokeo hayo ya mwisho, hapo katikati kuna mapambano makali sana.
Katika mapambano hayo, lazima damu zimwagike hasa.

Hakuna vita ambayo hakuna umwagaji wa damu.
Kwenye vita ya maisha damu utakazomwaga ni uchovu, kushindwa, kuumizwa, kusalitiwa, kupoteza na mengine mengi yanayokatisha tamaa.

Hayo ni mambo ya uhakika ambayo yapo kwenye hii safari, lakini wengi huwa hawajiandai nayo, hivyo yanapotokea wanajikuta kwenye mshangao mkubwa, maana ni kitu ambacho hawakutegemea.

Wewe usiwe kwenye kundi la aina hiyo, ingia kwenye vita ya maisha ukijua lazima damu zimwagike.

Na kama mwanajeshi mzuri, unajua fika kwamba kadiri utakavyotokwa jasho jingi wakati wa mazoezi, ndivyo utakavyotokwa damu kidogo wakati wa mapambano.

Kumbe basi mbadala wa damu ni jasho.
Kama hutaki utokwe na damu nyingi mwenye hii vita ya maisha, basi hakikisha unatokwa jasho jingi.

Unatokwa jasho jingi kwa kufanya mambo mapya, makubwa na magumu.
Unakuwa na malengo makubwa ambayo yanakusukuma kufanya zaidi ya ulivyozoea.

Ni katika kujituma kwako huko ndiyo unatengeneza fursa ambazo zinakukinga na mambo mbalimbali yanayowasumbua sana wengine.

Chagua kumwaga jasho jingi wakati wa mazoezi au kumwaga damu nyingi wakati wa mapambano.

Hatua ya kuchukua;
Kuwa na ndoto na malengo makubwa, kisha chukua hatua kubwa katika kuzifikia. Kadiri unavyofanya magumu kwenye maisha, ndivyo yanakuwa rahisi kwako.

Tafakari;
Ukifanya mambo rahisi, maisha yanakuwa magumu.
Na ukifanya mambo magumu, maisha yanakuwa rahisi.
Huwezi kukwepa huo ugumu, unachoweza ni kuuhamishia sehemu nyingine.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining