2730; Sumu inayoua taratibu.

Nikikuambia sasa hivi unywe sumu ambayo itakatisha maisha yako mara moja utanishangaa sana.
Utaniambia huwezi kufanya hivyo, kwa sababu bado unataka kuishi.

Lakini tukikuchunguza kwa kina, kwa namna unavyofanya mambo yako, tunaweza kuona huna tofauti sana na anayetumia sumu.
Tofauti pekee ni sumu unayotumia wewe inaua taratibu na hivyo madhara yake huyaoni tu haraka, ila yapo.

Ushahidi wa kwanza ni matumizi ya muda wako.
Tukimulika siku 7 zilizopita na kuorodhesha mambo yote uliyofanya tangu kuamka asubuhi mpaka kulala, ni mambo mangapi yatakuwa yenye tija kwako na mangapi ni ya kupoteza tu muda?

Muda ndiyo kipimo kikuu cha maisha yetu, kama unapoteza muda, unayapoteza maisha. Ni sumu inayokuua taratibu ambayo huwezi kuona madhara yake mara moja.

Ushahidi wa pili ni vitu unavyoingiza kwenye mwili wako. Hapa hasa ni kwenye vyakula na vinywaji.
Tukimulika siku saba zilizopita na kuangalia kila ulichokula na kunywa, huenda tutakutana na vitu ambavyo siyo bora kwa afya yako, lakini wewe mwenyewe umeviweka kwenye mwili wako.

Afya ndiyo mtaji mkuu kwenye maisha yako. Unapoichezea hovyo na kutokuijali, huna tofauti na kutumia sumu inayokuua taratibu.

Unaweza kusema unayapenda maisha, lakini matendo yako yakawa ni tofauti kabisa na hilo.
Matendo yako yakawa ni sawa na kutumia simu inayokuua taratibu.

Inapokuja kwenye maneno na matendo, matendo huwa yana nguvu zaidi.
Yafanye matendo yako yaonyeshe kweli unayapenda na kuyajali maisha.
Tumia vyema muda wako na linda sana afya yako, hivyo ni vitu viwili muhimu sana vinavyojenga maisha yako.

Hatua ya kuchukua;
Mulika maisha yako kwa siku 7 zilizopita na andika kila ulichofanya na kila ulichoweka kwenye mwili wako.
Kisha pitia kimoja kimoja na kuona kama kina manufaa au madhara kwako.
Kama utaendelea kufanya au kutumia kitu hicho kila siku, ndani ya miaka 10 kitakufikisha wapi?
Kama hakikufanyi kuwa bora zaidi miaka 10 ijayo, acha kukifanya mara moja.

Tafakari;
Unaweza kudanganya kwa meneno, lakini matendo huwa hayaongopi.
Kile unachofanya ndiyo uhalisia wako.
Kama unataka kujitathmini kweli, angalia yale ambayo umekuwa unafanya.
Hayo ndiyo yatakayokupa picha nzuru na ya uhalisia kuhusu wewe.

#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining