2734; Kama ungekuwa huogopi chochote.
Sehemu kubwa ya kikwazo cha watu kufanikiwa inatokana na woga ambao watu wanao.
Watu wanaogopa sana kushindwa, wanaogopa kukataliwa na wanaogopa wengine watawachukuliaje.
Kinachotokea ni watu kufanya mambo ambayo ni ya kawaida na yanayoficha woga wao.
Na hilo linapelekea washindwe kupata mafanikio makubwa.
Ili uweze kufanikiwa, unapaswa kuwa na ujasiri wa kutokuogopa chochote kile.
Lazima uwe tayari kufanya kila unachopaswa kufanya ili kufanikiwa.
Acha kufikiria utashindwa, kukataliwa au wengine watakuchukuliaje.
Wewe unajua unachotaka, kinachopaswa kufuata ni kukiendea mpaka kukipata.
Watoto wadogo huwa hawana woga kama ambao watu wazima wanao.
Huwa wanajua nini wanataka na nini hawataki na kuwa wazi kwenye hayo.
Unaweza kusema wanakuwa hivyo kwa sababu ya utoto.
Lakini unachosahau ni kwamba hiyo ndiyo asili yetu binadamu.
Woga ni kitu ambacho tumefundishwa.
Kwa asili tuna ujasiri mkubwa ndani yetu.
Wachache wanaogundua hilo na kuliishi ndiyo wanaopata mafanikio makubwa.
Huku wengi wanaodhibitiwa na woga wao wakiendelea kubaki kwenye hali duni.
Kwenye lile eneo ambalo umechagua kufanikiwa, usiogope chochote.
Amini kwenye fikra na maono uliyonayo na yasimamie mpaka kuyafikia.
Tumia ujasiri wako wa ndani kuchukua hatua kubwa na za kipekee ambazo zitakuwezesha kupata matokeo makubwa.
Ukivunja woga ulionao, mafanikio yatakuwa rahisi kwako.
Haimaanishi kwamba hutakutana na magumu, utakutana nayo sana, ila utaweza kuyavuka.
Woga ni sawa na breki kwenye safari ya mafanikio.
Kama umekanyaga breki za gari, haijalishi unakanyaga mafuta kiasi gani, bado gari hilo halitaweza kwenda kwa kasi kubwa.
Ni mpaka uachilie breki ndiyo gari itaweza kwenda kwa kasi kubwa.
Hatua ya kuchukua;
Jiulize ni mambo gani unayoyaogopa mpaka sasa kwenye safari yako ya mafanikio.
Hizo ndiyo breki ambazo umejiwekea kwenye hiyo safari na ndiyo maana inakuwa ngumu kwako.
Achilia breki zote kwa kutokuogopa chochote kwenye safari uliyochagua na utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.
Tafakari;
Kama kila binadamu ana uwezo mkubwa na wa kipekee ndani yake, iweje wachache ndiyo waweze kufanikiwa na wengi kubaki kwenye hali duni?
Jibu lipo kwenye woga, wanaoogopa ndiyo wanaoshindwa kwa sababu hawatumii uwezo wao mkubwa kufanikiwa.
Ipo kauli maarufu inayosema; woga wako ndiyo umasikini wako.
Ipo sahihi, ili kufanikiwa, hupaswi kuogopa chochote.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#We’reAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed