2736; Kujitoa nusu haisaidii.

Maandiko ya dini yanaeleza wazi kwamba ni bora kuwa moto au baridi, lakini siyo kuwa vuguvugu.

Kuwa vugu vugu hakukuweki kwenye upande wowote wa uhakika hivyo hunufaiki kwa namna yoyote ile.

Utanufaika zaidi kwa kujitoa kweli kweli kwenye upande mmoja, kuliko kujaribu kuwa kwenye kila upande.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye safari ya mafanikio.
Ni bora uamue kwamba utafanikiwa na kujitoa kweli kufanikiwa.
Au uamue hutahangaika na mafanikio na kwenda na maisha yako kwa mazoea uliyonayo.

Kutaka ufanikiwe wakati pia unaendelea na mazoea yako ni kujidanganya tu.
Kwanza unateseka kwa wakati unapojaribu kufanikiwa.
Halafu pia huipati raha ya kuwa kwenye mazoea maana unafanya kwa kuibia ibia.

Amua kujitoa kweli kwenye upande mmoja.
Kama ni wa mafanikio basi fanya kweli ili uweze kufanikiwa.
Usijizuie kwa namna yoyote ile.
Usiwe mtu wa kujaribu, bali kuwa mtu wa kufanya kweli kweli.

Na kama unaiona safari ya mafanikio ni ngumu kwako na haupo tayari kujitoa kwa ugumu huo.
Basi achana nayo na kaa kwenye mazoea hayo.
Usijaribu kabisa kuigiza kama vile upo kwenye safari hiyo ya mafanikio wakati hujajitoa kweli kweli.
Hakuna yoyote unayemdanganya zaidi ya kujipoteza wewe mwenyewe.

Hatua ya kuchukua;
Jiulize umejitoa kiasi gani kwenye safari yako ya mafanikio? Je umejiwasha moto kweli kweli wa mafanikio au upo vuguvugu?
Kumbuka vugu vugu haina matumizi yoyote.
Chagua kuwa moto kweli kwa kujitoa jumla jumla kufanikiwa.
Au kama unaona hilo halikufai basi achana kabisa na hiyo safari.

Tafakari;
Hakuna yeyote anayepata kitu kikubwa kwenye maisha yake bila ya kujitoa kweli kweli kwenye kitu hicho.
Kujaribu hakujawahi kumpa mtu matokeo makubwa.
Ni kufanya kwa kujitoa kweli ndiko kunakoleta mapinduzi makubwa kwa mtu.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed