#SheriaYaLeo (240/366); Jifunze kusikiliza kwa kina.

Chochote unachofikiria ni ambacho tayari unakijua.
Na yale unayojua ni machache mno ukilinganisha na mengi ambayo huyajui.

Unapokuwa unazungumza au kufikiria, akili yako ina tabia ya kuzunguka kwenye mambo yale yale ambayo tayari unayajua.

Lakini unapokutana na watu wengine, wanakuwa na vitu vya tofauti kwenye fikra zao ambavyo wewe huvijui.
Utaweza kuvijua vitu hivyo vya tofauti walivyonavyo watu kama utaweza kuwasikiliza kwa makini.

Kusikiliza kwa makini ni sawa na kuweza kuingia ndani ya fikra za mtu na kumwelewa kiundani.
Na kila mtu ana mengi ndani yake ambayo huwezi kuyajua kama hutasikiliza kwa umakini mkubwa.

Hata kwa watu wanaoonekana wajinga na wapumbavu, bado utajifunza mengi kuhusu wao kama utawasikiliza kwa makini.

Sheria ya leo; Jifunze kusikiliza kwa kina na utaweza kuingia ndani ya fikra za watu na kuwaelewa kwa undani. Kadiri unavyowaelewa watu kwa undani ndivyo unavyoweza kuwashawishi kwa urahisi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji