2738; Siyo lazima ufanye.

Sehemu kubwa ya msongo tunaokuwa nao kwenye maisha huwa ni wa kujitakia.

Tunakuwa na msongo pale tunapoona kwamba ni lazima tufanye vitu fulani ambavyo tumejiambia tunapaswa kufanya.

Ukweli ni kwamba hulazimiki kufanya kitu chochote kile.
Mahangaiko unayokuwa nayo kwenye kujilazimisha kufanya vitu, ni kujipa tu umaarufu ambao huna.

Hiyo ni kwa sababu, ikitokea umefariki dunia leo, hakuna chochote ambacho kitasimama. Dunia itaendelea kwenda kama inavyokwenda.

Pamoja na umuhimu unaojipa kwamba lazima ufanye vitu fulani, dunia haijali chochote kuhusu uwepo wako.
Maana uwepo au usiwepo, haiathiri mwenendo wa dunia.
Uwepo au usiwepo, ufanye au usifanye, haina tofauti yoyote kwenye mwenendo wa dunia.

Je hii inamaanisha kwamba tusifanye chochote kile, tujiendee tu na maisha kama minyoo?
Jibu ni hapana, lazima tufanye vitu vinavyoacha alama kwenye maisha, lakini hatupaswi kuruhusu chochote kutupa msongo.

Hatupaswi kuruhusu kitu chochote kitukoseshe amani na kutupa msongo pale tunaposhindwa kukifanya.
Kwa sababu siyo lazima tufanye chochote kile.

Tunapaswa kufanya kitu kwa sababu tumechagua na siyo kwa sababu tunalazimika kufanya.
Na hilo ndiyo linatuweka huru kuchagua wapi tuweke nguvu na umakini wetu ili kupata matokeo bora.

Ukiamua kuzima simu yako kwa siku nzima ili kupeleka umakini kwenye kitu ulichochagua, dunia haitasimama kwa sababu hupatikani hewani. Kila kitu kitaendelea kwenda kama kawaida. Huku na wewe ukiweza kufanya kilicho muhimu zaidi kulingana na ulivyochagua.
Msongo unaokuwa nao pale simu yako inapoisha chaji na ukawa hupatikani hauna maana yoyote.
Kwa sababu siyo lazima upatikane kwenye simu masaa yote 24 ya siku, siku 7 za wiki.

Siyo lazima upokee kila simu,
Siyo lazima ujibu kila ujumbe,
Siyo lazima uwe kwenye mitandao ya kijamii,
Siyo lazima usome kila kitu,
Siyo lazima ukubalike na kila mtu,
Siyo lazima umridhishe kila mtu.

Kwa kugundua kwamba siyo lazima ufanye chochote kile, jihadhari sana kwenye kukubali na kuahidi vitu.
Kubali na kuahidi kile kweli ambacho upo tayari kukijali kwa hali ya juu.
Vinginevyo ni bora tu kusema HAPANA.
Kwa sababu unajua HAPANA yako haitaisimamisha dunia.

Hatua ya kuchukua;
Ni mambo gani yanayokupa msongo mkubwa sasa kwa sababu unaona ni lazima uyafanye wakati haupo kwenye hali nzuri ya kuweza kuyafanya?
Jua kabisa kwamba siyo lazima uyafanye, ni maamuzi tu kwa upande wako.
Kwa kujua hilo utaweza kuondoa kabisa msongo wowote unaokuwa nao.

Tafakari;
Huwa tunapenda kujipa umaarufu na umuhimu tusiokuwa nao na hilo ndiyo linatuathiri sana kwenye maisha.
Msongo wowote tunaokuwa nao unatokana na kujilazimisha kwenye mambo ambayo siyo ya lazima.
Turudishe uhuru wetu kwa kujua hatulazimiki kufanya kitu chochote kile, badala yake ni uchaguzi wetu.
Hivyo tuchague kwa umakini na kufanya kwa ubora kwa sababu hatusumbuki na mengine.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed