2739; Hujashindwa, upo kwenye mchakato.
Mkulima A na B walikuwa na mashamba yanayopakana.
Wote walilima siku moja na kila mmoja kupanda mbegu zake kwa siku moja.
Baada ya siku 3, mbegu za mkulima A zikawa zimeota, ila za mkulima B zikawa bado.
Baada ya wiki, mkulima A tayari alikuwa na miche inayostawi, wakati mkulima B bado hata mbegu hazijaota.
Mkulima A alimcheka sana mkulima B, akimwambia mbegu alizootesha zilikuwa zimeharibika.
Muda unakwenda, wakati mkulima A anaanz kuvuna mazao, mbegu za mkulima B ndiyo zikawa zinaanza kuota.
Mkulima A aliendelea kumcheka na kumbeza mkulima B, kwamba anapoteza muda wake na ameshindwa.
Baada ya mwaka mkulima A ameshavuna mazao na kumaliza kabisa, wakati mkulima B ndiyo kwanza ana miche inayostawi.
Mwaka unaofuata na unaofuata mkulima A anarudia tena kupanda mbegu upya, wakati mkulima B anatunza miche yake.
Ni mpaka mwaka wa tatu ndiyo mkulima B anaanza kuvuna.
Na anaendelea kuvuna kwa zaidi ya miaka 10 bila kuhitajika kupanda upya.
Katika kipindi hicho, mkulima B ndiyo anaonekana kuwa na mafanikio.
Miaka mitatu ya mwanzo mkulima B alionekana kushindwa huku mkulima A akionekana kufanikiwa.
Ila miaka 7 iliyofuatia, mkulima B ndiyo alionekana kufanikiwa na mkulima A kushindwa.
Kufanikiwa na kushindwa ni misamiati ambayo imekuwa inatumiwa kwa namna isiyo sahihi.
Haijalishi wengine wanatumiaje misamiati hiyo, kwako futa kabisa msamiati kushindwa.
Kama bado unaendelea kupambana na kuweka juhudi, jua bado hujashindwa, bali upo kwenye mchakato wa kupata ushindi.
Hata kama hujayapata mafanikio au huyaoni kwa karibu, kamwe usikiri kushindwa.
Kwa sababu juhudi ndiyo zipo ndani ya udhibiti wako, matokeo hayapo.
Lakini kwa kuweka juhudi sahihi, lazima utapata matokeo sahihi.
Mbaya zaidi ni pale unapopima kushinda au kushindwa kwako kwa kujilinganisha na wengine.
Hakuna unayefanana na wewe.
Na kile unachokiona nje kwa watu siyo sawa na kinachoendelea ndani yako.
Wewe ni mshindi, umezaliwa kushinda.
Matokeo unayopata sasa ni kwa muda tu.
Kukaa kwenye mchakato sahihi wa ushindi lazima kutakupa ushindi mkubwa.
Hatua ya kuchukua;
Ni mambo gani kwenye maisha yako ambayo unaona kama umeshashindwa?
Futa huo msamiati kushindwa.
Jua mchakato sahihi kwenye kila jambo kisha kaa kwenye mchakato huo.
Ushindi ni swala la muda tu pale unapokaa kwenye mchakato sahihi.
Tafakari;
Mbegu zinaweza kufanana kwa nje, lakini ndani ni tofauti kabisa.
Usijilinganishe na yeyote kwa nje, kilicho ndani yako ni kikubwa na tofauti kabisa.
Lazima ukiishi ndiyo kiweze kujidhihirisha kwenye maisha yako.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed