2741; Mara 10.
Grant Cardone, kwenye kitabu chake na msingi wake mkuu wa mafunzo yake anaoita 10X, anaeleza kwamba njia pekee ya kupata ukuaji mkubwa ni kufikiri na kufanya mara 10 ya ulivyozoea kufanya.
Seth Godin, kwenye moja ya makala zake anazoandika na kutuma kwa wasomaji ameelezea kwamba chochote ambacho mtu anaweza kufanya mara moja, anaweza kufanya mara 10 pia.
Kama unaweza kufanya kitu mara moja, unaweza kukifanya mara 10 pia.
Na pale unapofanya kitu mara kumi, unajenga ujuzi na uzoefu mkubwa kwako.
Inakuwa rahisi kufanya na kuendelea kufanya.
Kama unaweza kumshawishi mteja mmoja kununua, basi pia unaweza kuwashawishi wateja 10 kununua.
Kama unaweza kufanya wema kwa mtu mmoja, unaweza pia kufanya wema kwa watu 10.
Kama unaweza kuingiza kipato cha kiasi fulani, unaweza pia kuingiza mara kumi ya kiasi hicho.
Juhudi zozote unazoweka sasa, unaweza kuweka mara 10 zaidi.
Na matokeo yoyote unayopata sasa, unaweza kupata mara 10 zaidi.
Kikwazo kikubwa cha mafanikio makubwa kwa wengi ni kuridhika haraka na pale walipo sasa.
Watu huwa na kiu kubwa ya mafanikio wanapokuwa wanaanza.
Lakini wakishafika hatua fulani, wanaridhika na matokeo wanayopata na kupunguza juhudi.
Wewe usiwe hivyo, kwa kila lengo kubwa unalofikia, weka lengo jipya ambalo ni mara 10 ya lile ulilofikia kisha pambana kufikia hilo pia.
Ukilifikia weka tena ambalo ni mara 10 zaidi.
Unaweza kujiuliza sasa mwisho utakuwaje?
Na jibu ni hakuna mwisho.
Kama upo hai, bado unaweza kufanya zaidi.
Hivyo futa mawazo ya kutafuta mwisho na badala yake kuwa na mawazo ya kuendelea kuwa bora zaidi kila wakati.
Hatua ya kuchukua;
Yaboreshe malengo yako yote kwa kupanga kufikia mara 10 ya pale ulipo sasa. Kila matokeo uliyonayo sasa, zidisha mara 10 na hilo linakuwa ndiyo lengo unalopambania.
Mtazamo huu wa mara 10 utakusukuma kufanya makubwa zaidi ya ulivyozoea kufanya.
Tafakari;
Hakuna kitu kinachoua mafanikio haraka kama mazoea.
Pale unapoweka mazoea kwenye kitu chochote ndiyo unavunja kila fursa ya kukua zaidi.
Ondoa kabisa mazoea kwenye maisha yako kwa kila mara kufikiri na kufanya mara 10 ya kile ambacho umeshafikia.
Mara 10 inaweza kuonekana kubwa, lakini unapofanyia kazi ni kitu kinachowezekana kabisa.
Na ndiyo njia ya uhakika ya ukuaji.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed