#SheriaYaLeo (248/366); Epuka vita zisizo na manufaa.
Siyo kila vita ni ya wewe kupigana.
Siyo kila pambano lazima ushinde.
Na siyo kila anayekukabili unapaswa kujibizana naye.
Wengi wanakutega uingie kwenye mitego yao ili kukuvuruga usiendelee na mikakati yako mikubwa.
Wanakuchosha na mapambano yasiyo na tija kitu kinachoondoa nguvu zako kwenye yale ambayo ni muhimu kwako kufika kule unakotaka kufika.
Hivyo mara zote kokotoa manufaa ya kila kitu kabla ya kujihusisha nacho.
Muda na nguvu zako ni rasilimali zilizo na ukomo, hupaswi kuzipoteza kwa mambo ambayo hayana matokeo makubwa kwako.
Kila unapojikuta kwenye mapambano ambayo hayana mwisho, kila wakati kuna jambo jipya linaibuka, jua umeingia kwenye vita isiyo na manufaa kwako.
Na hilo utaliona sana kwenye mambo yanayohusisha zaidi maneno kuliko matendo.
Hivyo njia bora ya kuepuka kuzama kwenye vita hizo zisizo na tija ni kuepuka kutafuta ushindi kwa maneno, badala yake kuutafuta kwa vitendo.
Onyesha badala ya kuongea, hiyo ina nguvu ya kukuepusha na yale yasiyo na tija.
Kama hakuna unachoweza kuonyesha, basi siyo muhimu kama unavyodhani.
Okoa rasilimali zako muhimu ili zisipotee kwenye hayo yasiyo na tija.
Sheria ya leo; Tengeneza ngazi ya vipaumbele vya maisha yako, kwa kuainisha yale yaliyo muhimu zaidi na yasiyokuwa muhimu. Kabla hujaingia kwenye pambano lolote, unarudi kwanza kwenye vipaumbele vyako na kuangalia kama ndiyo kitu muhimu kabisa kwako kufanya na kama ushindi utakuwa na tija.
Kama ni muhimu weka mkakati ambapo utaweza kushinda kwa vitendo na siyo maneno. Kama siyo muhimu achana nayo.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji