#SheriaYaLeo (255/366); Imani ya shujaa.
Asili huwa inaweka ukomo kwa kila kiumbe hai, ukomo wa mwisho ukiwa ni kifo.
Huwa tuna ukomo kwenye kiasi cha nguvu tunachoweza kutumia kabla hatujachoka.
Kadhalika kwenye muda na vipaji, tunavyo ila kwa ukomo mkubwa.
Samaki hawezi kuruka angali na wala ndege hawezi kuishi ndani ya maji.
Kila kiumbe hai huwa kina uimara na udhaifu wake.
Na hivyo kila kiumbe hupangilia jinsi ya kutumia uimara wake kwa tija ili kupata kile ambacho kinataka.
Simba ni mkali na mwenye nguvu, lakini hitamkuta akikimbiza panya.
Kwa sababu anajua kufanya hivyo ni matumizi mabaya ya nguvu zake.
Atachoka bure, atapoteza nguvu zake kwa kitu ambacho hakina tija kwake.
Kwa kujua hilo, simba hutunza nguvu zake kwa ajili ya mawindo yatakayompatia kitoweo.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwetu binadamu, tuna ukomo wa nguvu, muda na vipaji. Kuna maeneo tuna uimara na mengine tuna udhaifu.
Watangulizi wetu walijua vizuri hayo na kwa hatari ya maisha iliyokuwepo miaka mingi iliyopita, watu walikuwa wanapangilia vizuri kila wanachofanya.
Lakini kwa zama hizi ambapo hatari imepungua, watu wamesahau kupangilia vizuri rasilimali zenye uhaba kwao.
Ndiyo maana siku hizi watu wanapoteza muda na nguvu zao kwenye mambo yasiyokuwa na tija kabisa.
Mitandao ya kijamii kwa mfano, inawachosha wengi na kuchukua muda wao, lakini haina mchango wowote kwao kupiga hatua kwenye maisha yao.
Ni wakati wa kurudi kwenye uhalisia na kwenda na asili ilivyo.
Kuweka vipaumbele kwa usahihi ili kuweza kutumia vizuri rasilimali zenye uhaba tulizonazo.
Kuwa na imani ya shujaa ni kupangilia vizuri rasilimali muhimu.
Kuzitumia pale ambapo zina tija.
Na kuepuka kuzipoteza bure rasilimali hizo.
Huu ni mkakati bora wa maisha ambao utakutenganisha kabisa na watu wengine.
Mkakati unaokuwezesha kutumia rasilimali ulizonazo kwa tija kubwa.
Licha ya rasilimali hizo kubwa na ukomo, mkakati huo unakuwezesha kunufaika nazo.
Mashujaa huwa wanaweka mkazo kwenye yale wanayoweza kufanya na kuhakikisha wanayafanya kwa ubora wa hali ya juu.
Wanajua wakati wa kutumia rasilimali zao na wakati wa kuzihifadhi kwa matumizi bora zaidi ya baadaye.
Mkakati huo ndiyo unaowapa ushindi mkubwa wakati maadui zao wakijichosha na mambo yasiyo na tija.
Sheria ya leo; Kwenye mapambano yoyote yale, ni muhimu kupangilia vizuri matumizi ya rasilimali zako kwa namna ambayo utazitumia kwa tija kubwa. Kuna wakati ni bora kutokupambana kuliko kupambana na kupoteza rasilimali zako bila ya tija.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji