2753; Maumivu hayakwepeki.

Maisha yetu hapa duniani, tangu kuzaliwa mpaka kufa ni mwendelezo wa maumivu.

Zoezi lenyewe la kuja duniani ni la maumivu na ndiyo maana mtoto hulia anapozaliwa.
Na hata zoezi la kuondoka hapa duniani huwa ni la maumivu.

Katikati ya matukio hayo makubwa mawili, kuna mfululizo wa maumivu mengi ambayo mtu anayapitia kwa kipindi chote cha maisha yake.

Watu huwa na maisha mabovu pale wanapojaribu kuyakwepa maumivu.
Kwani hapo ndiyo hujikuta wakisababisha maumivu makubwa zaidi kwao na kwa wengine.

Kufanikiwa kuna maumivu, kadhalika kushindwa.
Utajiri una maumivu, lakini pia umasikini nao una maumivu yake.

Na hata pale unapotatua maumivu ya aina moja, jua unakaribisha maumivu ya aina nyingine.

Kwa maana hiyo basi, kuliko kuhangaika kutafuta njia ya kukwepa maumivu, isiyokuwepo, ni bora kuchagua maumivu ambayo upo tayari kwenda nayo.
Hayo ni maumivu unayoweza kuyakabili na kuyavumilia kwa kuwa unajua yanakuletea matokeo ya tofauti.

Hatua ya kuchukua;
Ni maumivu gani ambayo umeyachagua kwenye maisha yako?
Ni kipi upo tayari kukivumilia ili uweze kupata matokeo makubwa unayoyategemea?
Jibe majibu ambayo yatakuwa ndiyo mwongozo kamili wa maisha yako.

Tafakari;
Kwa kuwa maumivu ni sehemu ya maisha, kujaribu kuyakwepa maumivu ni kujaribu kuyakimbia maisha, kitu ambacho huwa hakina matokeo mazuri.
Usijipe matuaini hewa kwamba ukivuka maumivu fulani uliyonayo kinachofuata ni maisha ya raha mustarehe.
Maisha siyo hadithi za mwisho kuwa mzuri.
Maisha ni hadithi ya mwendelevu wa maumivu mpaka kifo.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed