2755; Unakimbilia wapi?
Hebu pata picha unapita njiani na kukutana na mtu unayemfahamu, anatembea kwa haraka sana.
Unamsimamisha ili kumsalimia anakujibu kwa haraka na kuendelea na kasi yako, anakuambia anataka kuwahi.
Unamuuliza kwani unawahi wapi?
Anakujibu hata sijui, ila nataka tu kuwahi.
Je utamwelewaje mtu wa aina hii?
Ni dhahiri utamwona amechanganyikiwa, ana haraka lakini hajui ni wapi anapotaka kuwahi.
Kabla hujakimbilia kumhukumu mtu wa aina hiyo, hebu kwanza jifikirie wewe mwenyewe.
Kwa haraka zote ambazo umekuwa nazo kwenye maisha yako mpaka sasa, zimekufikisha wapi?
Pale unaposema husomi kitabu kwa sababu huna muda, una mambo mengi ya kufanya, mambo hayo mpaka sasa yamekufikisha wapi?
Pale unapokataa kujaribu njia mpya ambazo zinaweza kukupa matokeo bora zaidi kwa kuona huna muda, kufanya ulivyozoea kumekufikisha wapi?
Kwa maisha yako yote umekuwa na haraka ambazo hazina tija kabisa.
Unahangaika na mambo ambayo hayana mchango wowote kwenye maisha yako.
Halafu unalalamika kwa nini unapata matokeo yale yale.
Ulitegemea upate matokeo gani kwa kufanya yale yale uliyozoea kufanya?
Kila unapokataa kujifunza na kujaribu nambo mapya, jiambie wazi kwamba unakimbilia usipopajua.
Haijalishi una haraka kiasi gani na unajipa sababu gani, jua unajidanganya tu.
Uhalisia utakukamata kwa namna mbio zako zitakuchosha na kukubakisha hapo hapo ulipo.
Wanaziita mbio za panya, hata ukishinda unabaki kuwa chanya.
Badala tu ya kuwa kwenye mbio, unapaswa kuanza na mkakati.
Wapi unataka kufika na njia ipi sahihi kupita.
Kukazana mbio huku hujui wapi unataka kufika na njia sahihi ya kutumia ni kujipoteza.
Sababu kuu ya kwa nini kwa miaka mingi umekuwa unahangaika sana ila hupati mafanikio makubwa ni hiyo, umekuwa na mbio za panya.
Hivyo kabla ya kuendelea na mbio hizo, ni lazima kwanza uache kuwa panya.
Lazima uwe na mkakati sahihi ambao kwa kila juhudi unazoweka zinakuwa na mchango wa kukufikisha kule unakotaka kufika.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kila unachofanya, jikamate kwa swali hili; ninakimbilia wapi? Pale unapojiambia huna muda wa kujifunza na kujaribu vitu vipya, jiulize ni wapi unakimbilia na hayo yaliyokutinga.
Kiuhalisia utagundua mengi unayohangaika nayo hayana tija yoyote kwako.
Tafakari;
Ni vyema kukaa kwenye mchamato sahihi. Unaweza kuonekana kama mchakato huo unakuchelewesha, lakini kwa uhalisia unakuwezesha kufanya makubwa kuliko kuendelea na mbio zisizokuwa na tija.
Wanasema sungura na haraka zake huishi miaka michache na kufa. Lakini kobe na utaratibu wake huishi miaka mingi na kudumu.
Unayajenga mafanikio yako kwa mtindo upi, wa sungura au kobe?
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed