2756; Unakulaje chakula kitamu?
Rafiki, kipi huwa ni chakula kitamu kwako na unachokipenda sana?
Je wakati wa kula chakula hicho huwa unaharakisha ukimalize haraka?
Upi ni mchezo au burudani unayopenda kufuatilia sana?
Je wakati unafuatilia mchezo au burudani hiyo huwa unataka kuharakisha ili kumaliza haraka?
Na je ni watu gani huwa unapenda sana kukutana nao na kufanya mazungumzo?
Je unapokutana na watu hao huwa unaharakisha mazungumzo yenu?
Unaipata picha rafiki yangu,
Vitu vyote bora kwetu na ambavyo tunavijali hasa, huwa hatuviharakishi.
Huwa tunavipa muda wa kutosha kwa sababu ni kupitia muda huo ndiyo tunanufaika na kufurahia vitu hivyo.
Halafu sasa unataka uharakishe kusoma vitabu.
Na tena unatafuta njia ya mkato ya kupata mafanikio na utajiri.
Unakazana kuharakisha kwenye kila kitu, kutafuta njia za mkato ambazo hazihusishi kazi wala muda.
Vitu vyote tunavyovifurahia, raha yake huwa haipo kwenye kuvikamilisha, bali raha huwa ipo kwenye mchakato wa kuvifanya.
Ndiyo maana wengi huona mafanikio na utajiri havileti furaha.
Furaha haipo kwenye matokeo, bali ipo kwenye mchakato.
Hukifurahii chakula baada ya kumaliza kula. Bali unakifurahia wakati unakila.
Kadhalika kwenye safari ya mafanikio na utajiri. Furaha haipo mwisho, bali kwenye mchakato mzima.
Hivyo basi, unapojikuta ukiharakisha, unapokuwa unatafuta njia za mkato, jua kuna shida mahali. Itakuwa vigumu kufanikiwa kwenye kitu hicho na hata ukifanikiwa hutayafurahia mafanikio hayo.
Hatua ya kuchukua;
Kila unapojikuta ukiharakisha kitu au kutafuta njia ya mkato, jiulize kama kitu hicho ndiyo muhimu kabisa kwako. Jikumbushe kinachokupa manufaa siyo matokeo, bali mchakato. Ukikaa kwenye mchakato sahihi ndiyo mafanikio yenyewe, bila hata kujali ni matokeo gani unayopata.
Tafakari;
Ukishajikuta unaharakisha jambo au kulitafutia njia ya mkato, jua wazi kuna tatizo mahali. Labda siyo jambo sahihi kwako au kama ni sahihi basi umelikabili kwa njia isiyo sahihi.
Manufaa ya kitu hayapo kwenye kukimaliza, bali kwenye mchakato mzima wa kukifanya. Tambua hili na ukae kwenye mchakato sahihi mara zote.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed