#SheriaYaLeo (260/366); Waondoe kwenye upande hasi.

Ni rahisi kukaa upande hasi kuliko upande chanya.
Ni rahisi kukosoa watu kuliko kuwasifia.
Ndiyo maana watu wengi huwa wanakimbilia kwenye huo upande hasi.

Inahitaji jitihada kubwa kukaa upande chanya na kueleza ubora wa kitu.
Ni rahisi kukaa upande hasi na kuonyesha udhaifu wa kitu.
Na pia watu huonekana wanajua pale wanapokosoa kitu.

Unapokabiliana na watu ambao wapo upande hasi, wajibu wako wa kwanza ni kuwaondoa kwenye upande huo hasi.
Kamwe usiwakabili watu wakiwa kwenye upande hasi, kwani watakushinda kirahisi sana.
Utakuwa umeingia kwenye uwanja wao wao na watakuangusha kwa urahisi.

Unachopaswa ni kuwapeleka kwanza kwenye upande chanya kwa kuhakikisha wanachagua kitu chanya, ambacho kinakupa wewe nafasi ya kuwakabili vizuri.
Na kama watakataa kukaa upande huo chanya, unaweza kuwakabili kwa huo ukaidi wao.

Sheria ya leo; Kwenye mapambano ya aina yoyote ile, epuka sana kumkabili adui kwenye uwanja wake. Kufanya hivyo utakuwa umejipeleka kwenye kushindwa. Badala yake unapaswa kubadili uwanja na kumpeleka adui kwenye uwanja wako, ambapo itakuwa rahisi kwako kumshinda.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji