#SheriaYaLeo (262/366); Mkakati wa hatua ndogo ndogo.
Tatizo kubwa ambalo watu wengi tunakabiliana nalo ni huwa tunakuwa na ndoto na matamanio makubwa.
Ndoto hizo kubwa zinateka hisia zetu kiasi cha kujikuta tunashindwa kuangalia hatua ndogo tunazopaswa kuchukua ili kufikia ndoto hizo kubwa.
Huwa tunapenda kufikiria hatua kubwa za kufikia ndoto tulizonazo.
Lakini kwa asili, kitu chochote kikubwa na imara huwa kinakuwa kimejengwa tararibu na kwa muda mrefu.
Mkakati wa kuchukua hatua ndogo ndogo ndiyo dawa pekee ya hali ya kukosa subira tunayokuwa nayo.
Mkakati huo unatufanya tuweke umakini wetu kwenye hatua ndogo kabisa tunazoweza kuanza kuchukua mara moja kuelekea kwenye ndoto zetu kubwa.
Kwa kupiga hatua moja baada ya nyingine ndiyo tunaweza kufika kwenye ndoto zozote kubwa tunazokuwa nazo.
Mkakati wa hatua ndogo ndogo pia unatulazimisha kufikiri kimchakato na siyo kimatokeo. Tunachokuwa tunaangalia ni hatua ndogo ndogo tunazoweza kuchukua na kuzichukua bila kujali matokeo.
Ni kupitia kuchukua hatua hizo ndogo ndogo ndiyo tunajikuta tukizalisha matokeo makubwa na kuzifikia ndoto zetu kubwa.
Hakuna kitu chenye manufaa kama kuchukua hatua ndogo ndogo kwa msimamo.
Mkakati huo una nguvu ya kukupa chochote unachotaka.
Sheria ya leo; Kuwa na ndoto na malengo makubwa unayotaka kuyafikia, lakini angalia hatua ndogo kabisa unayoweza kuanza kuchukua mara moja. Kufikia ndoto yoyote ile ni rahisi kama utaenda hatua kwa hatua.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji