2760; Mipango haifanyiki uwanjani.
Hebu fikiria timu ya mpira imeingia uwanjani kwa ajili ya mchezo wa fainali.
Wakati mashabiki wanaishangilia timu hiyo na kutegemea makubwa, kocha ndiyo anawakusanya wachezaji na kuwauliza tutumie mbinu gani kushinda?
Unajua kabisa timu ya aina hiyo itakuwa kwenye matatizo makubwa.
Kwani wakati wa mapambano siyo wakati wa kupanga mkakati gani wa kutumia.
Hilo linapaswa kuwa limefanyika mapema. Timu inakuwa tayari imeshamsoma adui na kujua madhaifu yake kisha kuweka mpango wa ushindi.
Timu inapofika uwanjani ni kutekeleza mpango ambao tayari umeshawekwa.
Hili ndiyo kosa ambalo wengi wanalifanya kwenye maisha, linalopelekea washindwe kufanikiwa.
Wengi wanakuwa hawana mikakati na mipango wanayoifanyia kazi.
Ni mpaka pale kitu kinapotokea ndiyo wanajiuliza wafanye nini kwenye hali ya aina hiyo.
Kama unasubiri mpaka ujikute kwenye matatizo au changamoto ndiyo ujiulize nini ufanye, tayari unakuwa umeshashindwa.
Unapaswa kuwa na mikakati na mipango unayoifanyia kazi nyakati zote, ili hata unapojikuta kwenye changamoto, hutaharuki, badala yake unaendelea na mchakato wako.
Uzuri ni unapokuwa na mikakati na mipango unayofanyia kazi, unapunguza matatizo na changamoto zisizo za lazima.
Na hata zile zinazokufikia, hazitakusumbua sana kwa sababu tayari unao mchakato sahihi.
Hatua ya kuchukua;
Jiulize kama unayo mipango na mikamati ya ushindi kwenye maisha, ambayo unaifanyia kazi kila siku.
Kama huna, hiyo ndiyo sababu ya kukwama, umekuwa unasubiri mambo yatokee ndiyo uone kipi utafanya.
Ni wakati sasa wa kubadilika, weka mikakati na mipango ambayo utakuwa unaifanyia kazi mara zote na kuiboresha kadiri unavyokwenda ili kujihakikishia ushindi mara zote.
Tafakari;
Kama huwa unasubiri matatizo au changamoto zikupate ndiyo uweke mpango wa kuzikabili, utaendelea kuishi maisha ya zima moto.
Kila wakati utakuwa umetingwa na mambo ya kutatua, lakini hakuna hatua kubwa unazokuwa unapiga.
Ni muhimu ukae chini na kutengeneza mkakati wako wa ushindi ambao utaufanyia kazi mara zote ili kupata ushindi mkubwa.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed