#SheriaYaLeo (268/366); Rudi nyuma kupata mtazamo mpya.

Tatizo kubwa linalotukabili kwenye mikakati na maisha kwa ujumla ni kwamba kila mmoja wetu ni wa kipekee kwa haiba yake.
Tunatofautiana sana na hata hali tunazopitia pia zinatofautiana.

Changamoto kubwa ni kwamba huwa hatuwezi kujua tofauti walizonazo wengine.
Mbaya zaidi ni tunashindwa hata kujua tofauti zetu wenyewe.
Wengi hawajitambui na kujua kile kinachowatofautisha na wengine.

Kwa maisha yetu yote tumekuwa tukifundishwa na wengine ya kuwa. Kuanzia kwa wazazi, walimu, jamii na hata vitabu. Yote hayo yamekuwa na ushawishi mkubwa kwetu kutufanya tuwe watu wa aina fulani.

Na hata pale mambo yanapotokea kwetu, huwa tunakimbilia kuyajibu kwa hisia na mihemko badala ya kuyatafakari kwa kina na kuyajibu kwa usahihi.
Matokeo yake yamekuwa ni kuharibu zaidi kuliko kujenga.

Wajibu wako mkubwa kama mwanamkakati ni kuona tofauti kati yako na watu wengine, kujijua wewe mwenyewe, upande wako na upande wa adui kwa kina kabisa.
Hilo litakusaidia kuweza kufanya maamuzi bora kabisa na yatakayokuwa na manufaa kwako.

Changamoto ni kwamba hili ni zoezi ambalo siyo rahisi, hasa ukizingatia mambo mengi tunayokabiliana nayo kila siku.
Na hapa ndipo unapokuja umuhimu w kurudi nyuma kidogo ili kuweza kupata mtazamo huo mpya.

Kama kila wakati unapambana na kushambulia, kila wakati unajibu watu kwa hisia na mihemko, hutapata muda wa kujenga mtazamo sahihi utakaokupa ushindi.
Mikakati yako itakuwa dhaifu kitu ambacho kitapelekea kushindwa.

Kurudi nyuma ili kupata mtazamo sahihi siyo kushindwa, bali ni kujiandaa na ushindi mkubwa zaidi.

Sheria ya leo; Kurudi nyuma siyo udhaifu bali ni uimara. Ni kitu unachopaswa kufanya mara kwa mara ili kuweza kujitambua na kujua tofauti yako na wengine kisha kuitumia vizuri.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji