2765; Halafu unafanya nini?

Rafiki,
Hii safari ya mafanikio huwa ni ngumu.
Lakini sasa, watu huwa wanazidisha ugumu wake mara dufu kwa mambo mbalimbali wanayofanya.

Moja ya mambo hayo ni kuwa na matarajio makubwa kuliko uhalisia.
Kitu ambacho kimekuwa hakifikiwi karibu mara zote.
Na hapo ndipo watu hukata tamaa.
Kwa kuona kama matarajio yao hayajafikiwa, basi hakuna haja ya kuendelea.

Rafiki, hayupo mtu yeyote aliyefanikiwa sana ambaye mara zote amekuwa anapata kila anachotaka kwa wakati anaotaka.
Hayupo kabisa.
Kila unayemwona amefanikiwa leo, alipitia magumu mengi, kushindwa, kukosa.
Kilichofanya afanikiwe ni uvumilivu na ung’ang’anizi katika kuendelea kufanya.

Usijidanganye kwamba mambo kwako yatakuwa tofauti, kwamba utaweza kupata kila unachotaka kwa wakati unaotaka.

Wewe hayo matokeo achana nayo, weka umakini wako kwenye nini unafanya.
Pale unapoweka juhudi kubwa na matokeo yakaja madogo, jiambie vizuri sasa, kisha jiulize nini unapaswa kufanya kwenye hali hiyo?

Ndiyo hivyo rafiki, kwenye kila matokeo unayopata, yawe makubwa au madogo, mazuri au mabaya, swali ni unafanya nini baada ya hapo.

Kama hakuna unachokwenda kufanya baada ya kupata matokeo fulani, umeanza kupotea.
Kama matokeo mabaya yamekukatisha tamaa,
Na kama matokeo mazuri yamekupa kuridhika,
Upo kwenye hatari kubwa.

Kila matokeo unayopata yanapaswa kuwa kichocheo kwenye kuchukua hatua za tofauti zaidi.
Ndivyo watu wamekuwa wakifanikiwa tangu enzi na enzi.
Na haitakuwa tofauti kwako pia.

Hatua ya kuchukua;
Kwa kila matokeo unayopata, jiulize swali; ninafanya nini baada ya hapa?
Kamwe usikubali matokeo yakukatishe tamaa au kukuridhisha.
Badala yake yatumie kama chachu ya kufanya zaidi ya hapo.

Tafakari;
Hakuna mafanikio yanayokuja kwa kufanya kile kile ulichozoea kufanya mara zote.
Mafanikio yanatokana na kufanya zaidi na tofauti ya ulivyozoea kufanya.
Kwa matokeo yoyote unayopata, panga kufanya zaidi na kwa tofauti.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed