#SheriaYaLeo (269/366); Epuka kukaa kwenye kona.
Kwenye michezo mbalimbali, kukimbilia kukaa kwenye kona ni kujipeleka kwenye kushindwa na hata kufa kabisa.
Hali hiyo pia ipo kwenye maeneo mengine ya maisha yetu.
Pale unapokabiliana na jambo lolote lile, kukimbilia kwenye kona ni kujipeleka kwenye kushindwa.
Kwenye kona kunaweza kuonekana kama ni sehemu salama.
Lakini inaishia kuwa sehemu hatari kwako kwa sababu adui anapokuzidi nguvu unakuwa huna pa kukimbilia.
Unakua umeondoa machaguo yako yote kitu ambacho kinamrahisishia adui kukumaliza.
Kukaa kwenye kona ni kupoteza machaguo mengi yanayokupa uhuru na kubaki na chaguo moja unaloona linakupa usalama, kitu ambacho kinakuja kugeuka kuwa hatari kubwa kwako.
Ni pale unapokuwa na njia moja tu ya kuingiza kipato na hivyo kumpa mtu anayedhibiti njia hiyo nguvu ya kukufanyia maamuzi.
Ni pale unapomtegemea mtu mmoja kwenye jambo muhimu kiasi kwamba asipokamilisha unakwama.
Kwa chochote unachofanya, epuka kukaa kwenye kona.
Hakikisha unabaki na machaguo mengi yanayokupa uhuru mkubwa.
Usikimbilie sana sehemu zinazoonekana ni salama, kwani zinaishia kuja kuwa mtego ambao utakutesa sana.
Mara zote angalia pale unakopata uhuru mkubwa, pale ambapo mtu mmoja au kitu kimoja hakiwezi kukukwamisha kabisa.
Mara nyingi kona ambazo watu wananasa ni vitu rahisi na vinavyolipa kwa haraka ambavyo havina nafasi ya ukuaji zaidi kwa baadaye.
Mara zote angalia picha kubwa ya baadaye na siyo manufaa ya haraka ya sasa.
Hilo litakuepusha kukaa kwenye kona ambayo inakuweka kwenye hatari kubwa.
Sheria ya leo; Wanamikakati huwa wanafikiri tofauti na jinsi ambavyo wengi huwa wanafikiri. Wakati wengine wanatafuta sehemu salama ambayo haitawasumbua, wanamikakati huwa wanatafuta sehemu yenye machaguo mengi ambayo inawapa uhuru mkubwa. Hilo linawaondoa kwenye kona na kuwapa fursa nyingi tofauti na wale wanaojiweka kwenye kona zinazoishia kuwa hatari kwao.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji