2766; Watu wasiokuheshimu.
Mtu mmoja amewahi kusema kwamba watu wengi kwenye maisha wanatumia fedha ambazo hawana, kununua vitu ambavyo hawavihitaji ili kuwaridhisha watu ambao hawajali.
Fikiria mtu anayekopa fedha, ili kununua gari ya kifahari kwa sababu anataka aonekane na wengine.
Naweza kwenda mbali zaidi na kusema matatizo mengi kwenye maisha yetu huwa yanatokana na watu ambao hatuwaheshimu wala kuwajali, ambao pia hawatuheshimu wala kutujali.
Wengi tunayaendesha maisha kwa mtazamo kwamba lazima tukubalike na kila mtu, lazima tujulikane na wote.
Hilo linatusukuma kufanya mambo ambayo yana gharama kubwa kwetu na wakati mwingine hata kutudhuru, ili tu kuwatidhisha watu ambao hatuwaheshimu na wala wao hawatuheshimu.
Unakuwa tayari hata kuiharibu biashara yako, kwenda kinyume na misingi ambayo umejiwekea wewe mwenyewe ili tu kumridhisha mteja, ambaye bado atakuacha na kwenda kwingine.
Unajitesa kwenye maisha yako, kufanya vitu ambavyo hupendi kufanya na vinakugharimu ili kumridhisha rafiki au mwenza wako, ambaye ikitokea fursa kidogo tu, labda umekosea kitu kidogo, anaachana na wewe mara moja.
Rafiki, kuna kitu muhimu sana cha kujifunza na kufanyia kazi hapa.
Tunapaswa kuyaishi maisha yetu kwanza kwa kujiheshimu sisi wenyewe, kisha kuambatana na wale wanaotujeshimu, ambao sisi pia tunawaheshimu.
Wanaokuheshimu wataelewa wapi unasimama na watakuunga mkono kwenye hilo.
Wataendelea kukuamini hata pale unapofanya makosa mbalimbali.
Wasiokuheshimu watadharau kile unachosimamia na kukutaka unadilike.
Na hata baada ya kubadilika, ukikosea wanaacha kukuamini na kuachana na wewe kabisa.
Kikubwa sana cha kuondoka nacho hapa ni usikubali kuvunja kile unachosimamia ili kuwaridhisha wengine.
Maana yeyote anayetaka uvunje unachosimamia ndiyo awe na wewe, bado atakuacha kwa sababu zisizokuwa na mashiko.
Watu wanaokuheshimu wanakupokea na kukubali vile ulivyo.
Na wanakupa ushirikiano wa kutosha kwa sababu wanajua kile wanachonufaika nacho kwako.
Hatua ya kuchukua;
Chunguz mahusiano yote uliyonayo, kuanzia binafsi, kazi na hata biashara.
Angalia ni yapi yamejengwa kwenye msingi wa kuheshimiana na yapi yamejengwa kwenye msingi wa kubembelezana.
Utagundua mahusiano yanayokutesa sana ni yale yaliyojengwa kwenye kubembelezana.
Amua sasa kuimarisha mahusiano yaliyojengwa kwenye kuheshimiana na achana na ya kubembelezana.
Tafakari;
Hakuna aliyekamilika,
Kila mmoja wetu ana uimara na mapungufu yake.
Watu wanapokushinikiza uwe namna fulani ndiyo wakukubali,
Ni watu wasiokuheshimu, ambao hata ukiwa wanavyotaka, bado hawatakukubali.
Simamia kile unachoamini na kilicho sahihi kwako na hapo utawavuta wale walio sahihi kwako.
Wengine achana nao, hawakuheshimu na huwaheshimu, haina haja ya kupotezeana muda.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed