#SheriaYaLeo (270/366); Achana na yaliyopita.

Kinachowakwamisha watu wengi ni kushindwa kuukabili uhalisia na kuona vitu jinsi vilivyo.
Kadiri tunavyokua kiumri, ndivyo tunavyozidi kufanya vitu kwa mazoea.
Tunatawaliwa zaidi na tabia.

Kitu ambacho kilitupa matokeo mazuri huko nyuma kinakuwa ndiyo msingi wetu, tunarudia hicho hicho kila wakati.
Marudio yanachukua sehemu ya ubunifu.

Huwa hatujigundui kuwa tunafanya hivyo, kwa sababu ni vigumu kwetu kuyaona mazoea.
Ghafla anatokea mtu ambaye hafuati mazoea wala kuheshimu desturi zilizopo.
Mtu huyo anafanya mambo kwa upekee na utofauti kabisa, kitu ambacho kinampa matokeo makubwa na kutushinda.

Hapo ndipo tunapogundua kwamba njia zetu zimepitwa na wakati.
Lakini unakuwa ni wakati ambao tumeshachelewa hivyo tunaambulia kushindwa.

Kamwe usiruhusu mazoea yakupeleke kwenye kushindwa.
Mafanikio yako ya nyuma siyo uhakika kwamba utaendelea kufanikiwa kwa kufanya yale uliyofanya.
Tena mara nyingi mafanikio ya nyuma ni kikwazo kwa mafanikio ya baadaye.

Kuepuka mafanikio yako ya nyuma kuwa kikwazo kwako, achana na yaliyopita na yakabili yajayo kwa namna ya kipekee.
Kila siku jifunze na kujaribu vitu vipya.
Kamwe usiende kwa mazoea.
Jua kilichokufikisha hapo ulipo sasa siyo kitakachokupeleka mbele zaidi.

Sheria ya leo; Chukulia akili yako kama mto, kadiri inavyotiririka kwa kasi ndivyo inavyoweza kukabiliana na mabadiliko yanayoendelea. Kukaa kwenye yale yaliyopita ni sawa na matope kwenye mto, yanapunguza kasi ya kutiririka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji