2767; Wanaheshimu unachokagua.
Umewahi kukubaliana kitu na mtu, kuhusu mambo anayopaswa kubadili.
Anakubali kabisa na anaanza kubadilika.
Lakini baada ya muda mfupi anarudi kule kule alikotoka.
Anayaacha mabadiliko na kurudi kwenye mazoea.
Unaweza kushangazwa na kuumizwa na hali ya aina hiyo.
Iweje mtu akubali kitu halafu baadaye abadilike?
Ambacho huelewi ni kwamba mabadiliko ni magumu.
Na hivyo watu wengi hupenda kukaa kwenye mazoea.
Hivyo watu hutafuta kila fursa ya kurudi kwenye mazoea, na pale nafasi ya kufanya hivyo inapojitokeza, wanaitumia vizuri kabisa.
Watu huwa wanakubali mabadiliko pale wanapokuwa hawana namna ila kubadilika.
Lakini kila mara hujaribu kurudi kwenye mazoea yao na kuona kama kuna madhara yoyote.
Wakijaribu kufanya hivyo na pasiwe na madhara, basi watarudi kwenye mazoea yao kidogo kidogo.
Hiyo ina maana kwamba, pale unapokubaliana na watu kubadili kitu fulani, unawajibika kuendelea kufuatilia kuhakikisha watu wanakaa kwenye mabadiliko hayo kweli.
Watu huwa wanaheshimu kile unachokagua na kufuatilia.
Wanaangalia unamaanisha kiasi gani kile unachotaka kwao.
Na mara kwa mara watajaribu kuyaacha mabadiliko waliyoyaanza.
Unapaswa kuendelea kusimamia mabadiliko ambayo mmekubaliana na mtu.
Kutokumwachia arudi kwenye mazoea.
Kuendelea kufuatilia na kukagua utekelezaji wa yale ambayo mmekubaliana.
Mabadiliko siyo rahisi kwa yeyote yule, hutamsaidia mtu kwa kumwacha apambane na mabadiliko yeye mwenyewe.
Badala yake unapaswa kumsaidia katika kutekeleza mabadiliko aliyoyakubali.
Kagua kila unachotegemea kwa watu na watakiheshimu na kukifanyia kazi.
Hatua ya kuchukua;
Kila unapokubaliana na watu kufanya mabadiliko fulani, usiwaache na kudhani wataendelea kubaki kwenye mabadiliko hayo wakati wote.
Badala yake endelea kuwafuatilia kwa karibu kuhakikisha kweli wanatimiza kile walichoahidi na kukubaliana nacho.
Siyo kwamba unakuwa unawalazimisha, bali unawasaidia wasikwamishwe na mazoea yao wenyewe.
Tafakari;
Mazoea ni magumu sana kwa mtu kuweza kuyabadili peke yake.
Kama hukagui matokeo unayoyategemea kwa watu, hakuna namna unaweza kuyapata matokeo hayo.
Kwani watu watarudi kwenye mazoea yao ya awali kwa urahisi kabisa.
Wasaidie watu waweze kuyavuka mazoea na kukaa kwenye mabadiliko waliyopanga.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed