#SheriaYaLeo (271/366); Jipe nafasi ya kubadilika.

Mradi wowote unaofanya, uwe ni sanaa, kazi au biashara ni sawa na kupigana vita.
Lazima uwe na mkakati wa jinsi unavyokabili tatizo, kupangilia kazi yako na kukabiliana na tofauti ya matokeo na mategemeo.

Watu wengi huwa wanaanza na wazo zuri, lakini katika kuweka mipango na kuitekeleza wanajiweka kwenye hali ambayo hawawezi kubadilika.
Wanajikuta wakifuata kile kile walichopanga kitu kinachowafanya wasifurahie wanachofanya wala kutumia fursa mbalimbali za mabadiliko.

Wakati mwingine watu wanaanza na wazo ambalo hawajalipangilia sana, ila wanaenda nalo hivyo hivyo bila kuliwekea mpango wowote.
Wanakuwa na uvivu wa kuweka mipango yoyote na kuendelea kuboresha, kitu ambacho kinapelekea washindwe kupata matokeo bora.

Suluhisho la hayo ni kuanza na wazo la kile unachotaka, kisha kujiweka kwenye nafasi ya wazi ambapo unaweza kufanyia kazi wazo lako na kuliboresha kadiri unavyokwenda.
Hiyo inamaanisha kutokujifungia kwenye hali ambayo itakuzuia kubadilika.
Inamaanisha kutokujiweka kwenye nafasi ambayo huna mahali pengine pa kwenda.

Hitaji hili ni la kimwili na hata kifikra pia. Unapaswa kuwa na fikra huru ili kuweza kutengeneza kitu chochote chenye thamani.

Sheria ya leo; Mara zote hakikisha una nafasi za wazi na siyo zilizojifunga. Pangilia kile unachofanya, lakini acha nafasi ya kuweza kubadilika pale fursa ya kufanya hivyo inapojitokeza.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji