2774; Wanajua usichojua.
Watu wote ambao wamefanikiwa zaidi kwenye maisha, kuna vitu ambavyo wanavijua ambavyo wasiofanikiwa hawavijui.
Kwa hao waliofanikiwa, wanaweza kuwa wanajua vitu hivyo kwa sababu ndivyo mtazamo wao ulivyo au kwa sababu wamepata nafasi ya kujifunza vitu vya tofauti.
Hivi karibuni nimesoma mahojiano ya msanifu majengo mkubwa, Frank Gehry, ambaye kwenye umri wake wa miaka 93 bado anaendelea kufanya kazi yake ya ufanisi, akifanya miradi mikubwa zaidi.
Kupitia maswali ambayo mwandishi alimuuliza, kuna mengi ya msingi ya kujifunza.
Lakini haya matano ya msingi kabisa ndiyo naona yana tija kubwa kwa kila mmoja kama atayafanyia kazi.
Moja ni ustaafu.
Mwandishi alimuuliza anaichukuliaje kazi yake ya mwisho.
Gehry alimjibu hiyo siyo kazi yake ya mwisho. Alieleza ataendelea kufanya miradi zaidi japo anajua mingi haitakamilika akiwa hai.
Tunajifunza kutokustaafu, badala yake tuendelee kufanya kile tunachopenda kufanya.
Mbili ni kuwa wewe.
Gehry anaeleza kila anapopata fursa ya kufundisha wanafunzi, huwa anawaambia wachukue karatasi na kuweka sahihi zao. Kisha anawaonyesha jinsi ambavyo sahihi ya kila mtu ni tofauti. Hivyo kila mtu anapaswa kubaki na utofauti wake.
Tunajifunza umuhimu wa kuwa sisi na siyo kuwaiga wengine.
Tatu ni msimamo kwenye kazi na siyo kufirahisha wateja.
Gehry anaeleza kuna baadhi ya kazi alipenda sana kuzifanya, lakini alitofautiana na wateja. Ila aliona ni bora azikose kuliko kujaribu kuwafurahisha wateja na kubaribu ubora na viwango vya kazi.
Tunajifunza umuhimu wa kuwa na viwango tunavyovisimamia na ambavyo hatupo tayari kuvivunja hata kama inatugharimu kukosa wateja.
Nne ni kutokukosoa wengine.
Pale mwandishi alipomuuliza Gehry anachukuliaje kazi za wasanifu wengine wakubwa alimjibu siyo sahihi kwake kuongelea kazi za watu wengine.
Tunajifunza umuhimu wa kuhangaika na mambo yetu ambayo ndiyo tuba uelewa nayo badala ya kuhangaika na mambo ya wengine.
Tano ni kupuuza wakosoaji.
Mwandishi pia alimuuliza Gehry anawachukuliaje wale wanaomkosoa yeye na kazi zake. Akamjibu hajui hata uwepo wa watu hao. Na kwa wale waliojaribu kufanya hivyo wazi wazi, hakuchukulia kama wanamshambulia yeye binafsi, bali aliona wana matatizo yao wenyewe.
Tunajifunza umuhimu wa kuweka umakini wetu kwenye kile tunachofanya na siyo kuhangaika na wale wanaotukosoa, maana hawatukusoi kwa sababu zetu, bali kwa sababu zao wenyewe.
Haya ndiyo mambo matano kati ya mengi ya kujifunza kutoka kwa msanifu huyu mkubwa. Unaweza kujifunza zaidi kupitia mahojiano hayo hapa; https://torontolife.com/real-estate/frank-gehry-has-a-few-things-to-get-off-his-chest/
Hatua ya kuchukua;
Katika haya matano ya msingi uliyojifunza hapa, unakwendaje kuyafanya kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku?
Tafakari;
Katika miaka yote ya ulimwengu, hapajawahi kutokea mtu kama wewe. Na wala hapatakuja kutokea mwingine kama wewe.
Wewe ni wa pekee na wa tofauti kabisa.
Lakini jamii haitaki uwe hivyo, inakazana kuhakikisha unafanana na wengine ili iweze kukutawala.
Kama unataka kufanikiwa kwenye maisha, hatua ya kwanza ni kuhakikisha unakuwa wewe kwenye hii dunia inayokulazimisha uwe kama wengine.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed