#SheriaYaLeo (279/366); Usiruhusu mafanikio yawe sumu kwako.
Sisi binadamu huwa tuna udhaifu ambao upo ndani ya kila mmoja wetu.
Udhaifu huo huwa unapelekea tujione na kujichukulia kwa namna ambayo siyo sahihi.
Udhaifu huo unatokana na asili yetu ya kupenda kujisifia na kukuza chochote tulichonacho.
Huwa tunaona tuna uwezo mkubwa kuliko wengine.
Ndani yetu huwa tuna tabia ya kujikweza kuliko wengine.
Huwa tunaona sisi ni bora zaidi ya wengine.
Tunajiona tukiwa na akili, uzuri, wema na hata umaarufu kuliko wengine.
Hali hiyo inaweza kuwa nzuri, kwani inatupa kujiamini na kutusukuma kufanya zaidi ya mazoea.
Tatizo huwa linaanzia pale tunapokuwa tumepata mafanikio.
Ni katika wakati huo ndiyo wengi wanalewa sifa za mafanikio na kuchukua hatua ambazo zinaishia kuwapa anguko kubwa.
Hiyo inasababisha mtu kuchukua hatua ambazo ni tofauti kabisa na uwezo wake halisi.
Sheria ya leo: Kila baada ya mafanikio unayopata, kaa chini na chambua kila kilochochangia kwenye mafanikio hayo. Ona mchango wa bahati na watu wengine katika kupata mafanikio uliyopata. Hiyo itakusaidia kuyaona mambo kwenye uhalisia wake na siyo kujidanganya.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji