#SheriaYaLeo (280/366); Ielewe Asili Yako.

Sisi binadamu tuna mambo mengi. Hatujui mawazo yetu yanatoka wapi. Wala hatujui hisia zetu zinatokea wapi.
Lakini tunaweza kuelewa vyanzo vya hayo kama tukiwa na udadisi na kuhoji maswali mengi.

Na hayo ndiyo matumaini pekee unayoweza kuwa nayo, kwa sababu ni vigumu kujua pale unapokuwa umetawaliwa na hisia zako.
Ni rahisi kujiona wewe ni zaidi ya wengine kutokana na maoni unayokuwa nayo. Unaweza kuruhusu upande wako mbaya kukutawala bila ya kujua.

Unapaswa kujua na kukubali kwamba asilimia 95 ya mawazo na maoni uliyonayo siyo yako, bali yametoka kwa watu wengine ambao wamekufundisha, umeyasoma mtandaoni au umewasikia watu wanasema au kuwaona wakifanya.

Kwa kifupi ni una tabia ya kuiga wengine na kufuata mkumbo.
Hivyo ndivyo binadamu wote tulivyo, hakuna aliye na afadhali.
Uzuri ni kwa kujua udhaifu wetu huo, inakuwa rahisi kuanza kuuvuka na kuhakikisha hauwi kikwazo kwetu.

Wajibu wako ni kudadisi na kuhoji kila kitu.
Usichukulie chochote kwa mazoea, bali taka kukielewa zaidi.
Ni kwa njia hiyo ndiyo utaweza kuifikia asili yako na kuzuia udhaifu wako usiwe kikwazo kwako.

Kufanya hivyo kutakusaidia uwaelewe watu kwa undani na kuacha kutegemea wawe kwa namna fulani.
Hayo yatafanya maisha yako rahisi na tulivu huku ukiwa na amani kwa sababu hakuna hisia zinazokuvuta chini.

Yote hayo yanaanza kwa kuangalia ndani na kujihoji maswali badala ya kudhani kila unachofikiri na kuhisi ni sawa.

Sheria ya leo; Jiulize, “Nilitoa wapi hii imani?” “Je ni kweli?” “Je ningekubaliana nayo kama ndiyo ningekuwa naisikia upya leo?”
Ni kupitia kudadisi na kujihoji ndiyo unaweza kuielewa asili yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji