2781; Watu na matatizo yao.
Mtu mmoja alisikia mbwa wa jirani yake akilia kwa uchungu na kwa muda mrefu.
Alishindwa kuvumilia na kuamua aende kuangalia nini kinaendelea.
Alipofika kwa jirani yake, alimkuta amekaa kwenye bustani yake akisoma gazeti, huku pembeni yake mbwa wake akiwa amekalia msumari ambao unamuumiza ndiyo maana akawa analia kwa uchungu.
Jirani yule alishangazwa na kumuuliza unakaaje kwa raha hivyo wakati mbwa wako analia kwa uchungu kutokana na msumari alioukalia?
Mtu yule alimjibu, kama huo msumari unamuumiza kweli, angeshaonendoka hapo, maana hajafungiwa kwenye huo msumari.
Baada ya kusema hayo aliendelea kusoma gazeti lake.
Jirani aliamua kurudi kwake.
Mfano huu unatupa funzo moja kubwa sana kuhusu watu wanaotuzunguka.
Kila anayetuzunguka na wa karibu kwetu ana matatizo yake mbalimbali.
Kuna wakati tunasukumwa kutaka kuyaingilia matatizo hayo ili kuwasaidia.
Lakini ni mpaka pale tunapojihusisha na matatizo ya wengine ndiyo tunajua ni kwa namna gani mambo kwa ndani ni makubwa na magumu kuliko yanavyoonekana kwa nje.
Tunaona matatizo waliyonayo watu wetu wa karibu tunapaswa kuwasaidia wayatatue, lakini tunaishia kuyageuza kuwa matatizo yetu, ambayo pia tunashindwa kuyatatua.
Tunapaswa kuwa makini sana na matatizo ya watu, hasa wale wa karibu kwetu.
Kama mtu ana tatizo linalomsumbua, kuna mambo mawili muhimu unapaswa kuyajua;
Kwanza ni kwa sehemu kubwa matatizo hayo anakuwa ameyatengeneza au kuyachochea yeye mwenyewe.
Na mbili ni hahangaiki sana kuyatatua.
Hivyo wewe unapokuja na kiherehere chako cha kutaka kuhakikisha unatatua matatizo yote ya wengine, unaishia kuyanunua matatizo hayo na yakaishia kukusumbua sana.
Hivyo basi rafiki yangu, unapaswa kuyaepuka sana matatizo ya watu. Kaa nayo mbali kabisa ili usije kuyanunua.
Na kama mtu hajakuomba umsaidie matatizo yake, kwa kuanza kuonyesha dhahiri hatua za makusudi anazochukua yeye mwenyewe kuyatatua, kaa mbali zaidi na matatizo ya mtu huyo.
Siyo kila mwenye matatizo anataka yatatuliwe, wengine wanatengeneza matatizo au kuyaacha ili kuyatumia kama sababu au visingizio.
Kwa kila anayekuzunguka na ana tatizo, anza kwa kuchukulia hivyo ili usije ukakimbilia kuyanunua matatizo yao.
Biashara yako kuu kwenye maisha inapaswa kuwa ni kujali mambo yako. Hilo haimaanishi usijali kuhusu wengine, ila epuka sana kujiingiza kwenye matatizo ambayo watu wanayo. Kuna sababu kwa nini watu wapo kwenye matatizo waliyonayo, huwezi kujua hiyo.
Hatua ya kuchukua;
Jiepushe sana kukimbilia kutatua matatizo ya wengine kwa sababu tu umeyaona. Hiyo ni njia rahisi ya kujinunulia matatizo.
Hapo ulipo tayari una matatizo ya kukutosha, hebu kwanza pambana na hayo na waache watu wa pambane na yao.
Kama mtu hajakuomba umsaidie kutatua tatizo lake, na kuonyesha wazi amejitoa kutatua, usijaribu kuingilia, utaishia kutengeneza matatizo zaidi kwako na kwa wengine.
Tafakari;
Matatizo ya watu yanasababishwa na vitu vingi ambavyo huwa havionekani kwa nje. Imani, mtazamo, ujinga, uvivu, uzembe na ushirikiano na wengine vina mchango sana kwenye matatizo anayokuwa nayo.
Wewe unapokimbilia kutaka kuwatatulia watu matatizo yao, unajipeleka kwenye kushindwa na kununua matatizo zaidi kwa ajili yako.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed