#SheriaYaLeo (288/366); Kabili upande wako mbaya.

Kila mmoja wetu ana upande wake ambao ni mbaya.
Kuna tabia fulani na madhaifu ambayo mtu unakuwa nazo ambazo umekuwa unajaribu kuvificha kwa sababu havikubaliki kijamii.

Kwa nje umejenga tabia na mwonekano ambao unafanya ukubalike na wengine na kuonekana mtu mzuri.

Ule upande wako mbaya ambao unakazana kuuficha, unahitaji nguvu kubwa kufanya hivyo.
Kuna wakati nguvu hiyo inazidiwa na unajikuta umeonyesha upande huo mbaya.

Hiyo inatokea pale unapokutana na kitu kinachokuchosha au kukupa msongo na kujikuta umesema au kufanya kitu kinachodhihirisha upande wako mbaya.

Unajikuta umewaumiza na kuwakwaza watu ambao ni wa karibu kwako kwa sababu tu umeshindwa kuficha upande wako mbaya.

Inaweza kuwa ni maneno uliyosema au hatua ulizochukua ambazo zinakuwa zimeishia kuwaumiza watu wengine.
Wakati unafanya unakuwa hujakusudia kabisa na unajisikia vibaya baada ya kuwa umeshafanya.

Hilo huwa linatokea kila unapokuwa na udhaifu ambao unasababisha ushindwe kuficha upande wako mbaya.
Inaweza kuwa pale unapokuwa na uchovu, hofu au hasira ndiyo unajikuta unasema au kufanya mambo ambayo yanawaumiza sana wengine.

Kuondokana na hilo, ni vyema kukabili upande wako mbaya badala ya kuuficha.
Kwa kuukabili unajua wazi kwamba una upande ambao siyo mzuri, upande ambao unapenda kuwaumiza wengine.

Unapoukabili upande wako mbaya, unaukosesha nguvu ya kukutawala na kuleta maumivu kwa wengine.
Unajua wazi nyakati ambazo ni rahisi kwako kuzidiwa na upande huo hasi na hivyo kuepuka kusema au kufanya mambo yanayowaumiza watu wengine.

Kitendo tu cha kukubali kwamba una upande mbaya ndani yako, tayari kinatosha kuunyima upande huo mbaya nguvu ya kukutawala, hasa pale unapokuwa na udhaifu.
Kuendelea kuficha na kukataa uwepo wa upande huo mbaya kunaupa nguvu ya kuendelea kuwaumiza wengine na hata wewe pia.

Sheria ya leo; Tambua na chunguza upande wako mbaya. Kwa kuuchunguza upande huo mbaya unaunyima nguvu ya kuleta uharibifu kwako na kwa wengine pia.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji