2785; Kuanza na kuendelea.

Mashine yoyote ile, huwa inatumia nishati kubwa zaidi kwenye kuanza kuwaka kuliko kuendelea kuwaka.

Chukua mfano wa injini ya gari au ndege, inapowashwa na kuanza safari inatumia mafuta mengi.

Lakini baada ya kuwaka na kuwa kwenye mwendo, mafuta yanayohitajika ili kuendelea na mwendo yanakuwa madogo kuliko yale ya kuanza.

Hivyo pia ndivyo inavyokuwa kwenye tabia zetu na maisha kwa ujumla.
Ni rahisi kuendelea kufanya kuliko kuanza kufanya.

Ni rahisi kuendelea kufanya mazoezi kuliko kuanza kufanya mazoezi.

Ni rahisi kutunza uzito wa mwili kuliko kupunguza uzito uliozidi.

Ni rahisi kutunza usafi wa nyumba kuliko kuisafisha nyumba chafu.

Ni rahisi kuendelea kujenga mahusiano kuliko kufufua mahusiano yaliyovunjika.

Ni rahisi kuendelea na biashara kuliko kuanza biashara mpya.

Ni kanuni ya asili na fizikia inayoeleza ni rahisi kwa kitu kubaki kwenye hali ambayo kipo mpaka pale nguvu ya nje inapobadili hali hiyo.

Kwa kujua nguvu ya kanuni hiyo, wewe unapaswa kutumia nguvu mwanzoni kujiweka kwenye mchakato sahihi unaokupeleka kwenye mafanikio yako.

Jiweke kwenye urahisi wa kuendelea kufanya kile unachopaswa kufanya badala ya kuanza upya kila wakati.

Chagua biashara unayoijenga ili kufika kwenye mafanikio yako na kaa kwenye biashara hiyo badala ya kila wakati kuwa unaanza biashara mpya.

Chagua tabia ambazo utakuwa unaziishi kila siku, mfano kuamka mapema, mazoezi, kujifunza na uendelee kuziishi badala ya kuanza tabia mpya kila siku.

Irahisishe safari yako ya mafanikio kwa kuhakikisha kila wakati upo kwenye mwendo badala ya kuanza na kuacha kila wakati.

Kila unapoacha unachofanya, inakuwa vigumu zaidi kwako kuja kuanza tena.
Hivyo kwa yale muhimu kwako kufanya, usikubali kuacha kuyafanya.
Unaweza kuona yanachosha kufanya, lakini ukiacha, inakuwa vigumu sana kwako kuja kuanza tena.

Hatua ya kuchukua;
Jiangalie wewe mwenyewe, ni mambo gani umekuwa unaacha kufanya na inakuja kuwa vigumu kwako kuyaanza tena japo ni muhimu?
Kwa kujua hilo, hakikisha hukubali kwa namna yoyote ile kuacha yale ambayo ni muhimu kwako kufanya.
Wewe fanya tu hata kama huyaoni matokeo sasa, maana ukiacha, kuja kuanza ni vigumu sana.

Tafakari;
Mazoea ni rahisi kuliko mabadiliko. Kwa kujua nguvu hiyo, unapaswa kujenga mazoea yanayokufikisha kwenye mafanikio yako. Jua kile unachotaka na jua unapaswa kufanya ninj ili upate unachotaka, kisha fanya kile unachopaswa kufanya bila ya kuacha. Mara zote kaa kwenye mwendo hata kama huyaoni matokeo.
Ni rahisi kuendelea kufanya kuliko kuja kuanza upya ukiwa umeacha.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed