2799; Meneja wa benki na biashara.

Taasisi zote kubwa, huwa zinawapa viongozi wake malengo ya namba ya kufikia kwa kipindi fulani.
Kuanzia mwaka, robo mwaka na mwezi.

Hapa nimetumia meneja wa benki kwa kurahisisha, lakini ndivyo ilivyo kwa kila taasisi kubwa.

Sasa tuendelee na mfano wa meneja wa benki.
Tuseme amepewa lengo la kufanya mauzo ya kiwango x kwa kipindi y.
Je unafikiri meneja huyo ataanza kuhangaika ni biashara gani afanye kupata mauzo hayo makubwa kwa haraka?

Je unadhani meneja huyo atashawishika na wale wanaokuja kumwambia kuna hii fursa mpya ambayo ukiweka fedha ndani ya mwezi inazalisha mara mbili?

Jibu ni hapana, meneja huyo atabaki kwenye biashara kuu ya taasisi.
Atakachofanya yeye ni kuangalia namna bora zaidi ya kuuza kile ambacho tayari ndiyo biashara kuu ya taasisi
Kuangalia jinsi ya kuwafikia wengi zaidi, kuwafanya wanunue na kuendelea kununua zaidi.
Na hapo ndipo mafanikio ya kiongozi husika.

Sasa turudi kwa wengi, ambao kila siku kuna fursa mpya wanahangaika nayo.
Leo unawakuta kwenye fursa hii, kesho wakisikia kuna fursa nyingine inayolipa zaidi wanaiendea.
Keshokutwa ikija fursa nyingine mpya zaidi unawakuta wapo pia.

Rafiki, kama na wewe upo kwenye huo mkumbo wa kila wakati kukimbizana na fursa mpya jua tayari umeingia njia ya kushindwa.
Utatawanya sana rasilimali zako muhimu kwa namna ambayo haiwezi kuwa na tija.

Hatua ya kuchukua;
Chagua biashara yako kuu ambayo ndiyo utaipa kila kitu chako mpaka ikupe mafanikio unayoyataka. Acha kukimbizana na fursa mpya kila wakati. Fursa kuu haipo kwenye upya, bali ipo kwenye ufanyaji wa kitu kwa muda mrefu, kukibobea na kupata matokeo makubwa.

Tafakari;
Kama taasisi kubwa, zenye timu kubwa ya watu na uwezo wa kila aina hazikimbilii hizo fursa ambazo watu wanaleta kwako kila siku, unadhani wanaoendesha taasisi hizo ni wajinga? Jifunze kutoka kwao, wanajua fursa kubwa ipo kwenye biashara yao kuu na hapo ndipo wanapoweka juhudi zao zote.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed