#SheriaYaLeo (303/366); Dhibiti majivuno yako.
Unataka kufanya makubwa na kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Umejiwekea malengo makubwa ambayo una uhakika wa kuyafikia.
Hayo yote ni mazuri kabisa na ndivyo wengi waliofanikiwa walivyofanya.
Ila kuna mahali pamoja wengi hukosea na hilo kupelekea kushindwa.
Wanapoweka malengo yao makubwa, wanaona ni lazima watayafikia.
Hawafikirii uhalisia wanaokwenda kukutana nao.
Ukweli ni kwamba kukamilisha kitu chochote kikubwa ni kugumu kuliko unavyoweza kudhani.
Mazingira yatakwenda kinyume na wewe, watu watakuwekea vizuizi na mengine mengi yatakukwamisha.
Wale ambao hawajajiandaa kwa hayo, wanapokutana nayo wanaishia kuwalaumu wengine kwa kuona ndiyo wamekuwa kikwazo kwao kupata wanachotaka.
Wanajiona wao hawana mchango kwenye kukwama kwao.
Hayo ndiyo tunayaita majivuno, kujiona wewe unapaswa kupata unachotaka bila kupitia magumu.
Kama hutajua na kudhibiti majivuno haya, kila wakati utakuwa unaishia kukutana na magumu na kushindwa.
Kwa lolote kubwa unalotaka kufanya, anza ukiwa unajua kabisa mambo yanakwenda kuwa magumu na ni rahisi kushindwa kuliko kushinda.
Kwa kujua hayo, utajipanga vyema na kuweza kuchukua hatua sahihi ili kuongeza nafasi za wewe kupata ushindi.
Sheria ya leo; Jua kabisa kwamba chochote kikubwa unachotaka kupata au kufikia kitakuwa kigumu kuliko unavyodhani. Anza na uhalisia huo ili uweze kuchukua hatua sahihi zitakazokuwezesha kupata unachotaka.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji