2805; Kujifunza na kazi.
Kama mtu yeyote akiniuliza ni vitu gani afanye ambavyo vitampa mafanikio kwa uhakika, bila ya kusita hata sekunde moja nitamjibu kujifunza na kazi.
Kujifunza kwa kina na endelevu kwenye kile ambacho mtu unafanya ni hitaji muhimu sana ili kufanikiwa. Unapaswa kukijua kweli chochote unachofanya, maana hivyo ndivyo utakavyoweza kufanya makubwa.
Kufanya kazi kwa juhudi kubwa ni hitaji jingine muhimu sana kuweza kufanikiwa. Mafanikio na kazi ni mapacha walioungana ambao hawawezi kutenganishwa kwa utaalamu wowote ule.
Ukijaribu tu kuwatenganisha mapacha hao, kinachotokea ni kifo.
Ni lazima uwe tayari kuweka kazi kwa juhudi kubwa ndiyo uweze kupata mafanikio makubwa.
Kama unaanzia chini kabisa na unataka kufanikiwa, unapaswa ujipe kiapo hiki; kwamba hakuna yeyote atakayekuwa anajua kile unachofanya kuliko wewe. Na hakuna yeyote ambaye atakifanya kwa juhudi kubwa kukushinda wewe.
Ni hivyo tu rafiki yako, wazidi wote kwenye kujifunza na kwenye kazi na matokeo utakayoyapata yatakuwa bora na makubwa kuliko ulivyodhani.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kile unachofanya, jiulize ni vitu gani ambavyo bado huvijui. Hakikisha unajifunza vitu hivyo kwa kina na kuelewa kuliko wengine wote wanaofanya hicho unachofanya.
Pia angalia kama juhudi za kazi unayoweka ndiyo za kiwango cha juu kabisa. Kama unaona ungeweza kuweka kazi zaidi, basi fanya hivyo, weka kazi zaidi.
Tafakari;
Waruhusu watu wakuzidi kwenye mambo mengine yote, fedha, uzuri, akili, koneksheni na mengine. Lakini usimruhusu mtu yeyote akuzidi kwenye mambo haya mawili; kujifunza na kazi. Jifunze na jua kile unachofanya kuliko wote wanaokifanya na kifanye kwa juhudi kubwa kuliko wengine wote wanavyokifanya.
#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed